LIVE STREAM ADS

Header Ads

Prof. Mwegoha aongoza waombolezaji kumuaga Balozi Dkt. Kamala

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha ameungana na ndugu, jamaa na marafiki kuuaga mwili wa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala aliyefariki dunia tarehe 12 Febuari 2024.

Prof. Mwegoha amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar- Dkt. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo- Prof. Saida Yahya Othman ambao kwa pamoja wamemwelezea marehemu Balozi Kamala kama kiongozi aliyekuwa na maono ya kimkakati katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa ndani na nje ya nchi, kujenga amani na kuleta maendeleo kwa Tanzania kupitia nyadhifa mbalimbali alizoshika enzi za uhai wake.

Ibada ya kuuaga mwili huo imeanyika Februari 17, 2024 katika Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko jijini Dar es Salaam.

“Tukio hili si jepesi kulipokea hasa ukizingatia mahusiano mema ambayo marehemu aliyejenga na wafanyakazi wenzake, wanafunzi na watu mbalimbali waliobahatika kukutana naye. Pia, ni pigo kubwa kwa jamii yetu na kwa nchi ya Tanzania kwa ujumla kupoteza kiongozi mwenye uzoefu na mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali hususan kwetu sisi wanataaluma” amesisitiza Prof. Mwegoha.

Amesema Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala atakumbukwa kwa mchango mkubwa kwa Chuo Kikuu Mzumbe toka alipokuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi (IDM-Mzumbe), akiwa mtu aliyeipenda sana kazi yake katika kuongoza kundi kubwa la wanachuo na kuajiriwa kama Mkufunzi mwenye ufahamu wa hali juu katika masuala ya Uchumi.

“Mchango wa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala bado unaishi na utaendelea kuishi kupitia kazi nyingi za kitaaluma na kisiasa alizozifanya. Moja ya vitu vinavyofariji ni sifa aliyokuwa nayo ya kupenda kuyaweka mawazo yake katika maandishi. Hii inatusaidia kubaki na rejea ya mambo aliyoyafahamu, vitu alivyoviamini na mawazo aliyoyajenga juu ya mambo mbalimbali” amesisitiza Prof. Mwegoha.

Awali, Paroko wa Kanisa la Mwenyeheri Isidori Bakanja Padri Emmanuel Makusalo na Padri Florence Rutaihwa Rwehumbiza kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania walioendesha ibada ya misa ya mazishi, kwa pamoja, wamewataka waamini na waombolezaji kujiandaa na kifo kwa kudumu katika sala ili waweze kukikabili vema kwa kuwa hakuna ajuaye siku wala saa.

No comments:

Powered by Blogger.