LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Nyamagana ataka usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya maendeleo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya hiyo (DCC).


Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya hiyo (DCC) ambapo ameahidi kuzisimamia taasisi zote ili kuhakikisha zinakuwa na matumizi mazuri ya fedha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Kikao hicho kimechofanyika Ijumaa Feburuari 16, 2024 kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka vyama vya siasa, Kamati ya Usalama ya Wilaya, Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji wa Kata, wadau wa maendeleo pamoja na viongozi wa dini.

Makilagi amesema taasisi zote za Serikali zinatakiwa kutekeleza kile ambacho kimepangwa kama ambavyo bajeti imepitishwa ili kupata thamani ya fedha itakayoleta matokeo chanya kwa ajili ya maendeo endelevu ya wananchi.

Aidha ameeleza kuwa maoni mbalimbali yaliyotolewa na wajumbe wa kikao hicho yatazingatiwa ili kuwa na bajeti chanya itakayowagusa wananchi wa Wilaya ya Nyamagana.

Akitoa taarifa ya makadirio ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa mwaka 2024/2025 kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Aron Kagurumujuli, Mkuu wa Kitengo cha Mipango na Uratibu, Edward Mwamotela amesema Halmashauri inaomba kuidhinishiwa kukusanya mapato ya ndani kiasi cha Tsh. 31,258,260,000.00 kutoka katika vyanzo mbalimbali ambapo mapato lindwa ni Tsh. 4,949,675,000 na mapato yasiyolindwa ni Tsh 26,308,585,00.

"Asilimia 70 ya mapato yasiyolindwa ni sawa na Tsh 18,416,009,500 ambazo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo na kiasi cha Tsh. 12,684,942,500 zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida" amesema Mwamotela.

Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyamagana, Geofrey Kavenga ametoa wito kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuendelea kukusanya mapato bila kuwabugudhi wafanyabiashara na kuhakikisha mapato hayo yanaenda kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Aron Kagurumujuli akizungumza kwenye kikao hicho.
Wajumbe wa Kamati ya Ushauri Wilaya ya Nyamagana (DCC) wakiwa kwenye kikao ambacho pamoja na mambo mengine kimejadili rasimu ya bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa mwaka 2024/25.
Wajumbe mbalimbali wa DCC Nyamagana wakifuatilia kikao hicho.

No comments:

Powered by Blogger.