LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mradi wa 'Green and Smart Cities' wazinduliwa Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Tawala Msaidizi Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa Mwanza, Patrick Kalangwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elkana Balandya kwenye uzinduzi wa mradi wa Green and Smart Cities uliofanyika Ijumaa Februari 20, 2024 jijini Mwanza.


Na Hellen Mtereko, Mwanza 
Mradi wa Green and Smart Cities (SASA Program) unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) kwa lengo la kuboresha miundombinu ya masoko na mialo ya samaki ili kuchochea fursa za kimaendeleo kwa wananchi umezinduliwa jijini Mwanza.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika Jumanne Februari 20, 2024 kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Halmashauri ya Jiji la Mwanza na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Idara, Madiwani na Wakurugenzi wa Halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela.

Mratibu wa mradi huo kutoka OR- TAMISEMI, Shabani Ally amesema mradi huo unatekelezwa katika Wilaya mbili za Mkoa wa Mwanza ambazo ni Ilemela na Nyamagana ambapo Umoja wa Ulaya (EU) umetoa msaada wa Euro Milioni 75 ambazo zimeingia kwenye bajeti ya Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia kutekeleza miradi mbalimbali.

Amesema Serikali ya Tanzania inaangalia maeneo ambayo yanaboresha mnyororo wa thamani kwenye chakula hivyo wanahitaji maeneo ya masoko, machinjio na mialo ya samaki yawe na ubora kwa ajili ya kuimarisha uchumi na afya kwa wananchi.

"Tutaboresha maeneo ya kuhifadhia vyakula kwenye masoko, wavuvi tutawasaidia kupata mbinu bora, tutaboresha machinjio na mengine yatabomolewa kwa ajili ya kuanza usanifu na kujengewa upya" amesema Ally.

Aidha ameeleza kuwa baada ya kujenga na kuboresha miundombinu hiyo, Serikali na Umoja wa Ulaya wataendelea kutoa mikopo kwa vijana na wanawake ili waweze kupata fedha za kukuza biashara zao.

Amesema mradi huo utaboresha miundombinu ya maji kwa kuongeza mtandao ya maji ili wananchi wote wapate maji safi ambapo eneo hilo linafadhiliwa na shirika la maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Naye Mratibu wa Programu ya Green and Smart Cities kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Martino Jinci amewahimiza  viongozi mbalimbali wakiwemo waliohudhuria uzinduzi huo ukiwajibika ipasavyo ili kuhakikisha mradi unaleta tija ya maendeleo kwa wananchi na kwamba hawapaswi kuona mradi huo kama kitu cha ziada bali kama sehemu yao ya kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Kiomoni Kibamba amesema mradi huo utaongeza fursa ya kibiashara kupitia ujenzi wa soko la Buswelu na kuboresha ukuzaji wa uchumi kutokana na kuongezeka kwa fursa za kibiashara na kupunguza upotevu wa chakula.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Peter Lehhet amesema katika awamu ya kwanza ya mradi huo, kipaumbele kwao ni miradi miwili ambayo ni ukarabati wa machinjio ya Nyakato na ujenzi wa soko la Buhongwa ambapo miradi hiyo ikikamilika itaongeza mapato yatakayowawezesha kuongeza miundombinu ya elimu na afya.

Awali akizindua mradi huo, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Viwanda, Biashara na Uwekezaji- Patrick Kalangwa amesema utaimarisha utekelezaji wa mpango kabambe wa (Jiji Master Plan) pamoja na kuendeleza maeneo ya wazi (green spaces).

Kalangwa ametoa wito kwa viongozi kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa ipasavyo kwani Serikali inatarajia kuona matokeo chanya ya miradi iliyoainishwa hatua itakayosaidia utekelezaji wa miradi zaidi nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Peter Lehhet akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi wa Green and Smart Cities.
Mratibu wa Mradi wa Green and Smart Cities kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Martino Jinci akielezea namna mradi huo utakavyosaidia kukuza uchumi kwa wananchi.
Viongozi mbalimbali wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa mradi wa Grean and Smart Cities jijini Mwanza.
Viongozi mbalimbali na wadau wa maendeleo wakifuatilia uzinduzi wa maradi wa Green and Smart Cities uliozindiliwa jijini Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.