LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wafanyakazi TANESCO wakumbushwa kufanyaka kazi kwa maadili, kuepuka rushwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wafanyakazi wa shirika la umeme nchini (TANESCO) Kanda ya Ziwa wamekumbushwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma huku wakijiepusha na vitendo vya rushwa katika kuwahudumia wananchi.

Rai hiyo imetolewa Jumatano Aprili 24, 2024 jijini Mwanza na Afisa Rasilimali Watu TANESCO Kanda ya Ziwa, Eliza Mlangwa wakati akizungumza kwenye warsha ya kutoa elimu kwa wafanyakazi wa shirika hilo mkoani Mwanza kuhusu rushwa na maadili kabla ya kusaini fomu ya maadili ya utumishi wa umma.

Mlangwa amesema kila mfanyakazi wa umma anapaswa kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuepuka viashiria vya rushwa kazini hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwakumbusha wajibu huo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gisima Nyamhanga ambaye alitaka mafunzo ya aina hiyo kutolewa nchi nzima.

Amesema mafunzo hayo yametolewa kwa wafanyakazi wa TANESCO katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na wafanyakazi kusaini fomu ya maadili ya utumishi wa umma hivyo ni matarajio wafanyakazi wa TANESCO watatumia elimu waliyoipata kuendelea kutoa huduma bora isiyo na viashiria vya rushwa kwa wateja.

Naye Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa Mwanza, Mhandisi James Kabasa amesema hategemei kuona wafanyakazi wa shirika hilo wakiingia katika mtego wa vitendo vya rushwa kwani elimu waliyoipata imewakumbusha hatua zinazoweza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi ambapo shirika limeona ni vyema kutoa elimu hiyo kwa wafanyakazi.

Akiwasilisha mada kwenye warsha hiyo, Afisa wa TAKUKURU Mkoa Mwanza, Maua Ally amesema huduma ya nishati ya umeme ni msingi wa maendeleo kwa Taifa hivyo ni vyema wafanyakazi wa TANESCO wakajiepusha na vitendo vya rushwa na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi.

Baadhi ya wafanyakazi wa TANESCO akiwemo Mhandisi Deus Bubelwa na CPA. Paulina Nondi wamesema elimu ya maadili na rushwa itawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi, bila kushawisha na vitendo vya rushwa na kuhakikisha wateja wanapata huduma bora.

Katibu wa chama cha wafanyakazi (TUICO) Mkoa Mwanza, Martine Wawa amesema hatua ya TANESCO kuwakumbusha wafanyakazi wajibu wao itasaidia kuleta matokeo chanya katika utumishi na kuwaepusha na changamoto zinazoweza kuhatarisha ajira zao.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG 
Afisa Rasilimali Watu TANESCO Kanda ya Ziwa, Eliza Mlangwa akizungumza kwenye warsha ya kutoa elimu kwa wafanyakazi wa shirika hilo kuhusu masuala ya rushwa na maadili ya kazi.
Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa Mwanza, Mhandisi James Kabasa akizungumza kwenye warsha ya kutoa elimu kwa wafanyakazi wa shirika hilo kuhusu masuala ya rushwa na maadili.
Afisa wa TAKUKURU Mkoa Mwanza, Maua Ally akizungumza kwenye warsha ya kuwajenga uelewa wafanyakazi wa TANESCO kuhusu masuala ya rushwa na maadili ya kazi.
Afisa wa TAKUKURU Mkoa Mwanza, Maua Ally akitoa elimu kuhusu masuala ya rushwa na maadili ya kazi kwa wafanyakazi wa TANESCO kutoka Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (TUICO) Mkoa Mwanza, akizungumza na wafanyakazi wa TANESCO na kuwahimiza kuzingatia maadili ya kazi na kujiepusha na viashiria vya rushwa.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (TUICO) Mkoa Mwanza, akizungumza na wafanyakazi wa TANESCO na kuwahimiza kuzingatia maadili ya kazi.
Afisa Maadili Sekretarieti ya Maadili a Viongozi wa Umma, Roseline Mugasha akitoa elimu kuhusu maadili kwa wafanyakazi wa TANESCO mkoani Mwanza kabla ya kusaini fomu ya maadili ya kazi.
Afisa Maadili Sekretarieti ya Maadili a Viongozi wa Umma, Roseline Mugasha akiwaongoza wafanyakazi wa TANESCO mkoani Mwanza kula kiapo cha maadili ya viongozi wa umma kabla ya kusaini fomu ya maadili ya kazi.
Afisa Rasilimali Watu TANESCO Kanda ya Ziwa, Eliza Mlangwa (kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TANESCO Mkoa Mwanza, Emmanuel Matuba (kushoto) wakisaini fomu ya maadili ya kazi wakati wa warsha hiyo.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.