Mwanza na jitihada za kupambana na magonjwa ya watoto
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Ingawa Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano,mkoa wa Mwanza bado unaendelea na jitihada za kupambana na magonjwa mbalimbali ya watoto yanayosababishwa na ukosefu wa chanjo pamoja na saratani
Kutokana na utafiti uliofanywa na hospitali ya rufaa ya kanda ya Bugando kuhusu saratani kwa watoto ulibaini kuwa kwa mwaka 2009 watoto 50 waligundulika kuwa na saratani na mwaka 2023 watoto wenye saratani waliongezeka na kufikia 300 ambalo ni ongezeko kubwa.
Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya saratani ya watoto na damu hospitali ya rufaa ya Bugando, Heronima Kashaigili amesema hatua mbalimbali za matibabu ya saratani kwa watoto zilianza kuchukuliwa kuanzia mwaka 2023-2024 baada ya kuona ukubwa wa tatizo hilo.
Dkt. Heronima amesema baada ya kuanza mikakati ya kutibu kansa kwa watoto waligundua watoto wengi wanasumbuliwa na saratani ya matezi,saratani ya misuli,saratani ya damu,saratani ya ubongo,saratani ya macho na saratani ya mifupa.
“Kwa mwaka 2009 watoto 50 waligundulika na saratani na Ufanisi wa kuwatibu ulikuwa chini ya asilimia 20 zaidi ya watoto 35 walikuwa wakifariki lakini kufikia mwaka 2023 watoto 300 waligundulika kuwa na saratani na ufafanisi wa matibabu umefikia zaidi ya asilimia 50 kwa hiyo kuna maendeleo mazuri” alisema dkt Heronima.
Mkurugenzi hospitali ya rufaa ya kanda Bugando, Dkt. Fabian Masaga anasema pamoja na kuanza kutoa matibabu hayo kwa watoto wadogo gharama ya matibabu ni kubwa na ili waweze kuokoa maisha ya watoto wanashambuliwa na saratani wameamua kuwashirikisha wadau ili wakusanye fedha za kupambana na saratani ya watoto hasa kwa watoto ambao familia zao hazina uwezo.
Serikali imewekeza nguvu kubwa katika hospitali ya Bugando hasa upande wa matibabu ya saratani na kupelekea hospitali ya Bugando kuwa kituo cha matibabu ya saratani kwa kanda ya ziwa.
Mbali na jitihada hizo za kupambana na saratani ya watoto Mkoa wa mwanza haupo nyuma katika kupambana na magonjwa ya watoto yanayozuilika kwa chanjo, mkoa umekuwa na kampeni mbalimbali zinazoendelea zikiwa na lengo la kuhakikisha kila mtoto anapatiwa chanjo ya kumkinga na magonjwa mbalimbali yanayozuilika kwa chanjo.
Makilagi amesema kwa mwaka wa fedha 2022-2023 mkoa ulifanikiwa kuwachanja jumla ya watoto 205,0394 sawa na asilimia 107 kati ya walengwa ambao walikadiriwa kuchanjwa watoto 191,0440 wenye umri wa chini ya mwaka mmoja.
Amesema kwa mwezi februari 2024 mkoa wa ulitekeleza kampeni ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa surua na rubella na kufanikiwa na kufikia ufanisi wa asilimia 106 ambapo watoto 808,433 waliweza kuchanjwa kati ya watoto kati ya watoto waliokuwa wamewalenga 762,858 wenye umri chini ya miaka mitano walichanjwa.
Makilagi amesema mwezi machi 2024 mkoa wa Mwanza uliendesha kampeni maalumu ya utoaji wa chanjo kwa watoto wote ambao hawajachanjwa na walio nyuma ya ratiba ya chanjo zao na kufanikwa kuwachanja watoto 37,213 ambao kati yao watoto walikuwa 4302 sawa na asilimia 14.
Kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kampeni mbalimbali za chanjo mkoani Mwanza kunachangizwa na mashirika yasiyo ya kiserikali kuendesha kampeni mbalimbali za uhamasishaji chanjo kwa watoto.
Mkurugenzi shirika la Dunia Rafiki Sophia Asenga anasema hivi karibuni wao kupitia kituo chao cha Malezi na Makuzi ya Mtoto waliendesha zoezi la chanjo na upimaji uzito kwa watoto waliopo kwenye kituo hicho na wale ambao wanaotoka mitaani.
Sophia amesema kwa kutambua umuhimu wa chanjo,utoaji wa dawa za minyoo pamoja na upimaji uzito kwa watoto waliamua kuendesha zoezi hilo kwa watoto wa kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi miaka minne.
“Ili mtoto aweze kukua katika utimilifu wake katika Nyanja zote ni lazima mtoto apatiwe chanjo ili kumkinga na magonjwa na tunapowapima uzito inasaidia kujua maendeleo ya ukuaji wa mtoto na kama mtoto akionyesha dalili ya kudumaa basi moja kwa moja tutajiuliza upande wa lishe unaweza kuwa na mapungufu hivyo tutaongeza virutubisho” alisema Sophia.
Wizara ya afya kupitia kitengo cha kinga imesema mapambano dhidi ya magonjwa ya watoto yanayozuilika kwa chanjo yamekuwa yakifanyika kila mwaka hapa nchini kwa lengo la kuhakikisha watoto wote wanakua katika ukamilifu wao.
Waziri wa afya Ummy Mwalimu amesema chanjo sio jambo geni hapa nchini kwa kuwa lilianza tangu kipindi cha Mwalimu Julias Nyerere ambapo chanjo 3-4 zilitolewa na kwa hivi sasa chanjo 10 zinatolewa kwa watoto ili kuwakinga na magonjwa mbalimbali yanayotibika kwa chanjo.
Kuhusu changamoto ya baadhi ya wazazi kutowapeleka watoto kupatiwa chanjo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo suala la umbali wa vituo vya afya na ukosefu wa elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa chanjo kwa watoto,waziri Ummy amewataka wazazi kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo ya pili ya surua pamoja na chanjo nyingine muhimu.
Ummy amewataka wazazi wenye watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote kwa mujibu wa ratiba hasa chanjo ya Surua ambayo hutolewa mtoto akiwa na umri wa miezi 9 na dozi ya pili baada ya miezi 18 ambapo wazazi wengi hawarudi kwenye vituo vya afya ili kupata dozi ya pili ya Surua.
Nae mzazi Joseph Elisha mkazi wa mtaa wa Nganza ameitaka srikali kuendelea kutoa elimu kuhusu dalili mbalimbali za magonjwa ya watoto ili wao kama wazazi waweze kuwahi katika vituo vya afya kwaajili ya matibabu kabla ugonjwa haujawa mkubwa na kusababisha madhara kwa mtoto.
Jitihada hizi za kupambana na magonjwa mbalimbali ya watoto zinazofanyika jijini Mwanza zinaendana na lengo la program jumuishi ya taifa ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto upande wa afya ambapo kila mtoto anatakiwa kupatiwa matibabu na kukingwa na magonjwa yote yanayoweza kumzuia mtoto kukua katika utimilifu wake.
Mpango jumuishi wa taifa wa malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto unahimiza umuhimu wa kuzingatia afya ya mtoto,wazazi wengi wamekuwa wanasubiri mpaka mtoto anapougua ndio suala la afya ya mtoto kutazamwa na wengine kusahau suala la afya hali inayosababisha ulemavu,udumavu na vifo vya watoto wadogo.
No comments: