DC Ukerewe ahimiza wananchi kuoga maji ya bomba badala ya ziwani
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa wilaya ya ukerewe Christopher Ngubiagai amekemea tabia ya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kuoga kwenye fukwe za Ziwa Victoria badala ya kutumia maji safi ya bomba.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa vyombo vya utoaji wa huduma ya maji ngazi ya jamii pamoja na wadau wa maji wilayani humo, Ngubiagai alisema utamaduni wa kuoga ziwani uchi wa mnyama umepitwa na wakati.
Ngubiagai aliwahimiza wakazi wa Ukerewe kutumia maji ya bomba ili kuoga kwa staha badala ya kudhalilisha utu wao.
“Bado ustaarabu wetu ni mdogo sana, kuoga ziwani ustaarabu ule umepitwa katika karne hii, mnaweza kuona wazungu wengi wanakuja kwenye Wilaya hiii, kumbe wanafurahia kuona vile viungo kule ziwani na wanapiga picha na kupeleka kule ulimwenguni”alisema Ngubiagai.
Mkuu huyo wa Wilaya pia alisema kuoga ziwani kumekuwa chanzo cha ongezeko la maradhi ya milipuko pamoja na uchafuzi wa mazingira na kuwataka viongozi katika ngazi zote kuelimisha jamii kuhusu athari hizo.
Naye Meneja wa RUWASA Wilaya ya Ukerewe Mhandisi Zubeda Saidi alisema miradi tisa ya maji inayotekelezwa na Serikali wilayani humo kwa gharama ya shilingi billioni 18.8 itaongeza upatikanaji wa maji safi safi kufikia asilimia 89 ifikapo Disemba mwaka 2025.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Elisante Kimaro alieleza kuridhishwa na miradi ya maji safi inayotekelezwa kupitia RUWASA ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya chama hicho inayotaka huduma ya maji safi kuwafikia asilimia 85 ya wananchi waishio vijijini ifikapo mwaka 2025.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA>>> BONYEZA HAPA KUSOMA ZAIDI
No comments: