Meya wa Tulsa Marekani arejea Mwanza kukagua maeneo ya uwekezaji
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mstahiki Meya wa Jiji la Tulsa lililopo Jimbo la Oklahoma nchini Marekani, George Bynum amewasili jijini Mwanza, ili kukagua maeneo yaliyoanishwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo baina ya majiji hayo mawili.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili jijini Mwanza Jumatano Mei 29, 2024, Mratibu wa Mahusiano ya Miji Dada kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Billy Brown alisema Meya huyo ni mara yake ya pili kutembelea jijini Mwanza tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya Jiji la Mwanza na Jiji la Tulsa.
"Meya alipoondoka alituachia kazi Kamati ya Tulsa na Jiji la Mwanza kubaini maeneo ya kushirikiana, hadi sasa maeneo hayo ni elimu, afya, uchumi, uwekezaji, biashara, michezo, utamaduni na kilimo. Maeneo hayo yatawezeshwa kupitia ufadhili ambao tunategemea kuupata kutoka Tulsa Oklahoma" alisema Brown.
Alieleza kuwa zoezi kubwa ni kupitia na kufahamu maeneo ambayo wameshakubaliana ili kutengeneza mpango wa upatikanaji fedha, ufadhili wa miradi na shughuli za maeneo waliyoyaainisha.
Naye Naibu Meya wa Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha alimuomba Meya wa Jiji la Tulsa kusaidia sekta ya michezo hususani vifaa vya michezo kwa ajili ya kuiwezesha timu ya Pamba Jiji pamoja a kuboresha uwanja wa michezo Nyamagana.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Tulsa, George Bynum aliahidi kuendeleza ushirikiano na Jiji la Mwanza katika sekta mbalimbali ikiwemo michezo.
"Jiji la Mwanza mna timu ya Pamba Jiji na sisi Tulsa tuna timu inaitwa FC Tulsa, hivyo tutashirikiana kwa ukaribu ili tuzidi kuziboresha timu hizi" alisema Bynum.
Awali akizungumza baada ya kumpokea Meya wa Tulsa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda alisema Mkoa huo ni salama kwa uwekezaji ukizungukwa na fursa mbalimbali za utalii ikiwemo kisiwa cha Saa Nane na hivyo ushirikiano wa majiji ya Tulsa na Mwanza utaleta tija.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mstahiki Meya wa Jiji la Tulsa, George Bynum akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza.
Mstahiki Meya wa Jiji la Tulsa, George Bynum akizungumza baada ya kuwasili jijini Mwanza.
Mstahiki Meya wa Jiji la Tulsa, George Bynum (kushoto) akipokea jezi ya timu ya soka ya Pamba Jiji kutoka kwa Naibu Meya wa Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha (katikati). Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba.
PIA SOMA>>> MEYA WA TULSA AWASILI MWANZA
No comments: