Madiwani Mwanza waibua tena changamoto ya uhaba wa madawati
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza limebainisha kuwa bado baadhi ya shule za Sekondari na msingi zina upungufu wa madawati na hivyo kuiagiza Serikali kutatua changamoto hiyo ili kuondoa adha ya wanafunzi kukaa chini.
Hayo yalijiri Jumatano Juni 12, 2024 kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo, kilicholenga kupokea na kujadili taarifa za Kamati kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2023/24.
Diwani wa Kata ya Lwanhima, Marco Swalala alisema shule zilizoko kwenye Kata yake ikiwemo shule ya msingi Lwanhima zina uhaba wa madawati huku zikiwa na idadi kubwa ya wanafunzi.
"Shule ya msingi Lwanhima inajumla ya wanafunzi 1,600, madawati ni 102. Hii ni kero kubwa kwa wanafunzi kwani wanakaa kwa kubanana na wengine wanakaa chini. Serikali iangalie namna ya kushughulia changamoto hii" alisema Swalla.
Akizungumzia shule ya msingi Bugayamba iliyopo katika Kata ya Lwanhima, Swalala alisema ina wafunzi 780 huku madawati yakiwa ni 84.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Kishiri, Haruna Maziku alisema Kata hiyo ina upungufu mkubwa wa madawati karibia shule zote za msingi na sekondari.
Akijibu hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Peter Juma alikiri kuwepo kwa upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari na kwamba tayari hatua za kukabiliana na changamoto hizo zimeanza kuchukuliwa.
"Tumeona tuweke muda wa masomo uwe mara mbili, wanafunzi waingie asubuhi na watoke mchana. Wengine waingie mchana hadi jioni kwenye shule ambazo zina upungufu wa madawati" alisema Juma.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kushughulikia changamoto ya uhaba wa madawati kwani imekuwa ikijirudia.
Mara kadhaa Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kukabiliana na uhaba wa madawati katika shule za msingi na sekondari lakini changamoto hiyo imekuwa ikikosa suluhisho la kudumu kutokana na namba ya wanafunzi kubadilika kila mwaka huku baadhi ya madawati yakiharibika na kutofanyiwa ukarabati.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Diwani wa Kata ya Luchelele, Vicent Lusana akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
No comments: