LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la Fadhili Teens Tanzania laadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Fadhili Teens Tanzania limeungana na wadau mbalimbali wa kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto, kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika iliyoambatana na kutoa elimu kwa jamii ili kuwalinda mtoto.

Maadhimisho hayo yamefanyika Alhamisi Juni 13, 2024 katika Kata ya Nyasaka Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, ambapo kilele cha Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika Juni 16 kila mwaka.

“Tumepata fursa ya kutoa elimu kwa jamii na kwa wanafunzi wa shule za msingi Muungano na Nyasaka pamoja na shule ya sekondari Nyasaka ili kutambua jinsi ya kujilinda na vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini pia kutoa taarifa wanapobaini vitendo hivyo” amesema Sarah Emmanuel ambaye ni Mratibu mradi wa Msichana Thabiti unaotekelezwa na shirika la Fadhili Teens Tanzania.

Mwenyekiti wa Chipukizi Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela, Iqra Kweka ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho, amesema Siku ya Mtoto wa Afrika ni muhimu katika kuikumbusha jamii kutowatendea watoto vitendo vya ukatili.

Nao baadhi ya wanafunzi wametumia maadhimisho hayo kutoa rai kwa jamii kutovumilia vitendo vya ukatili hususani kwa watoto.

Maadhimisho hayo yameanza kwa maandamano kutoka eneo la Mnadani Nyasaka Centre hadi uwanja wa shule ya msingi Nyasaka huku yakipambwa na mashindano mbalimbali ya watoto ikiwemo kuvuta kamba na kukimbia na magunia huku washindi wakijipatia zawadi.

Siku ya Mtoto wa Afrika iliidhinishwa na Umoja wa Afrika kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa Kijiji cha Soweto nchini Afrika Kusini, waliouwawa wakati wa utawala wa makaburu, wakipinga vitendo vya ukatili na ubaguzi katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu ambapo pia imekuwa ikitumika kuikumbusha jamii kuwalinda watoto.

Wadau waliohudhuria maadhimisho hayo ni pamoja na viongozi wa dini, Serikali za Mitaa, Kata, wanafunzi, waalimu, wazazi, na mabalozi wa SMAUJATA ambapo kaulimbiu ya mwaka huu inasema “elimu jumuishi, izingatie maadili, maarifa na stadi za kazi”.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.