Mwanza wavutiwa na mkaa mbadala
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katika maonesho ya jamii, jiko lililokuwa na mkaa mbadala uliotengenezwa kwa mabaki ya mpunga liliivisha chakula haraka kuliko aina nyingine ya mkaa ukiwemo uliotengenezwa kwa magogo ya miti.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Wakazi wa jiji la Mwanza hasa wanawake wamevutiwa na matumizi ya mkaa mbadala unaotengenezwa kwa kutumia mabaki ya pumba za mpunga, wakisema aina hiyo ya mkaa inafaa zaidi kuliko ile inayotengenezwa kwa kutumia magogo ya miti.
Akizungumza baada ya kutumia mkaa huo, Rachel Yohana ambaye ni mkazi wa Buswelu alisema amevutiwa kwa namna mkaa huo mbadala unavyowaka haraka, bila kutoa moshi huku ukichelewa kuisha na hivyo kufanya kiwango cha matumizi kuwa kidogo na kumpunguzia gharama za kununua mkaa mara kwa mara.
“Huu mkaa mbadala niliutumia kuchemshia maharage, kwa muda mfupi yakaiva na nikaendelea kupika wali bila kuongeza mkaa mwingine. Natamani kuona mkaa huu unapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu kuanzia shilingi elfu moja” alisema Rachel.
Naye Mary Mwita mkazi wa Buzuruga alisema ni muda mwafaka sasa wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya kuuza mkaa mbadala hasa unaotengenezwa kwa kutumia pumba za mpunga kwani mikoa ya Kanda ya Ziwa inalima kwa wingi zao hilo hivyo kuna urahisi wa kupata malighafi hiyo.
“Nililetewa huu mkaa na mme wangu, akaniambia kuna shirika linautengeneza kwa majaribio. Sitamani kutumia mkaa wa miti maana unatoa moshi, pia unawahi kuisha hata kabla chakula hakijaiva” alisema Mary.
Kwa upande wake Upendo Binagi mkazi wa Kisesa alitoa rai kwa wadau wa mazingira kuendelea kutoa elimu kwa wazalishaji wa mkaa kuepuka kukata miti na kugeukia pumba za mpunga kwani mkaa wake utakuwa na soko zaidi kutokana na ubora wake.
Mkurugenzi wa shirika la uhifadhi la Peace For Conservation (PFC) la jijini Mwanza, David Kabambo alisema shirika hilo limekuwa likihamasisha matumizi ya mkaa mbadala (Briquette Charcoal) kama nishati safi ya kupikia na kuachana na tabia ya kukata miti kwa ajili ya kuni ama kutengenezea mkaa.
Sehemu ya mkaa wa majaribio uliozalishwa na vijana waliopewa elimu na shirika la Peace For Conservation (PFC) la jijini Mwanza.
Alisema kupitia ufadhili wa shirika la kimataifa la Environmental Education and Conservation Global (EECG), walitekeleza mradi wa majaribio wa kutoa elimu kuhusu uzalishaji wa mkaa mbadala kwa kutumia maganda ya mpunga (pumba) ambapo uzalishaji wa majaribio umepokelewa vizuri na watumiaji.
Kabambo alisema shirika hilo lilitoa mashine na kuwajengea uwezo vijana wa kiume na kike 40 ili kuzalisha mkaa mbadala kwa kutumia pumba za mpunga huku pia wanawake wajasiriamali 10 wakijengewa uwezo ili kuanza biashara ya kuuza mbadala utakaozalishwa na vijana hao.
“Tumekuja na kauli mbiu ya ‘mkaa bora, chakula bora’ ili kuhamasisha matumizi ya mkaa mbadala kwa ajili ya kupikia. Tunafurahi jamii imetambua kwamba maganda ya mchele yanaweza kutumika kama chanzo bora cha nishati ya kupikia na hivyo kuacha tabia ya kukata miti ovyo kwani tunatamani kuona Tanzania inakuwa ya kijani” alisema Kabambo.
Kabambo alisema mradi huo wa majaribio uliotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2023/24 umeongeza soko la mkaa mbadala unaotengenezwa kwa kutumia pumba za mpunga, hivyo shiika la PFC linafanya jitihada za kupata ufadhili ili kuwajengea uwezo mkubwa zaidi wazalishaji wa mkaa huo ili kukidhi mahitaji kwa kuanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Wakati wa utoaji elimu kwa jamii, Mkurugenzi wa shirika la uhifadhi la Peace For Conservation (PFC) la jijini Mwanza, David Kabambo (kushoto) alipata fursa ya kuonja ugali uliopikwa na mkaa mbadala uliotengenezwa kwa mabaki ya mpunga.
No comments: