LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wafanyabishara Pwani wahimizwa kuzingatia usafi wa mazingira

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wafanyabishara katika soko la Bwilingu, Halmashauri ya wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, wametakiwa kuzingatia utunzaji na usafi wa mazingira katika soko hilo.

Wito huo umetolewa Juni 29,2024 na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe wakati wa uzinduzi wa soko hilo.

Dkt. Kapologwe amesema miundo mbinu ya soko la Bwilingu ni mizuri sana hivyo Wafanyabiashara wana jukumu la kufanya usafi wa Mazingira na kulinda miundo mbinu hiyo.

"Miundombinu iliyojengwa katika soko hili inalenga katika udhibiti wa taka ngumu pamoja na taka miminika katika eneo hili ambapo wameweza kujenga vyoo ambavyo vinatumika na wafanyabiashara wa soko hili" amesema.

Ameeleza kuwa kampeni ya Mtu Ni Afya, yenye kauli mbiu ya 'Fanya kweli, usibaki nyuma' imejikita katika suala la usafi wa mazingira pamoja na usafi wa mtu mmoja kama unawaji wa mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka.

Dkt. Kapologwe amesema pia kampeni hiyo imekuja kuhamasisha jamii suala zima la kufanya mazoezi.

"Mazoezi yanasaidia sana katika kuimarisha mwili na kupambana dhidi ya magonjwa ambayo sio ya kuambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu" amesema.

Amemwagiza Mwenyekiti wa soko la Bwilingu, Shabaan Saidi kutengeneza sehemu malumu ya kunawia mikono kwa wafanyabiashara na watu mbalimbali wanaofika katika soko hilo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kapologwe ameitaka jamii kuzingatia ulaji uliobora na kuepuka suala la kutumia sukari nyingi katika chakula.

Naye Mkurugenzi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Ramadhani Possi amesema kampeni ya Mtu Ni Afya, imewasaidia sana katika kuhamasisha kampeni ya kunawa mikono kwa maji tiririka ambayo halmashauri hiyo ilikuwa imeanzisha kampeni hiyo.

Amesema Halmashauri yao imetumia shilingi milioni 90 katika ujenzi wa vyoo vya kisasa katika soko la Bwilingu. Possi amesema Halmashauri yao imenunua gari malumu la kubebea takataka kwajili ya kufanya usafi na utunzaji wa Mazingira.

Mratibu wa Afya, Uzazi na Mtoto Wilaya ya Chalinze Beatha Mchopa amehimiza wafanyabiashara kwa ujumla pamoja na wakazi wa Wilaya ya Chalinze kuwa na utaratibu malumu wa kunawa mikono.

Akielezea kuhusu Hedhi salama,Mchopa amewashauri wazazi kujenga utaratibu malumu wa kuwafundisha watoto wao kuhusu hedhi salama.

"Watoto wanapokuwa katika kipindi cha balehe, wanatakiwa kujifunza namna gani ya kuishi katika hedhi salama. Walimu mashuleni pamoja na wazazi watambue mtoto anapoingia kwenye hedhi mtoto anatakiwa kutumia kitambaa salama na anatakiwa kujua jinsi ya kuhifadhi hivyo vitambaa na kukusanya na kuchoma moto" amesema.

No comments:

Powered by Blogger.