Wafanyabiashara soko la mbugani walalamikia ubovu wa miundombinu
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wafanyabiashara katika soko la Mbugani jijini Mwanza, wamelalamikia ubovu wa miundombinu katika soko hilo, hali inayosababisha wapate hasara kutokana na bidhaa zao kuharibika hasa wakati wa mvua.
Baadhi ya wafanyabiashara katika soko hilo wameyasema hayo Mei 30, 2024 wakati wakizungumzia changamoto zinazowakabili ikiwa imepita zaidi ya miaka mine tangu wahame kutoka soko kuu kupisha ujenzi wake.
“Tunapoteza mali kiholela, maeneo mengine yanavuja mvua ikinyesha kiasi kwamba wengine wamefirisika na kuacha biashara. Pia usalama ni mdogo hasa usiku, vibaka wanaingilia popote maana soko halina mageti” alisema Abdulkarim Mohamed, mfanyabiashara wa soko hilo.
Pia wafanyabiashara wengine, Tatu Kwiro na Faustine Fidelis walisema wakati wa mvua soko hilo linakuwa sawa na ziwa kutokana na maji kuzagaa kila mahali hali inayosababisha pia wateja kutoenda sokoni hapo kutokana na adha inayokuwepo.
Mmoja wa wafanyabiashara katika soko la Mbugani, Abdulkarim Mohamed.
Mmoja wa wafanyabiashara katika soko la Mbugani, Tatu Kwiro.
Mwonekano wa baadhi ya vizimba katika soko la Mbugani.
Mwenyekiti wa soko kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika soko la Mbugani, Hamad Nchola amekiri soko hilo kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kiusalama, ubovu wa miundombinu na kutofikika kwa urahisi na kwamba suluhisho la changamoto hizo ni kukamilika kwa soko kuu ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 94.
“Tulipisha ujenzi wa soko kuu mjini kati Septemba 28, 2019 na mara zote huwa nawaambia wafanyabiashara tuwe watulivu kwani baada ya muda mfupi tutarudi kwenye soko jipya la mjini kati” alisema Nchola.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa Mwanza, Said Mtanda ametoa ahadi ya kufuatilia kwa ukaribu ukamilishaji wa ujenzi wa soko kuu jijini Mwanza, biashara zifanyike katika mazingira rafiki na salama.
“Nilituma timu yangu ikiongozwa na RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) kufuatilia hazina fedha zilizoombwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambazo ni shilingi bilioni tatu, zitakapofika mimi na viongozi wenzagu tutashinda hapa kuhakikisha asilimia sita za ujenzi zilizobaki zinakamilika ili mhamie kwenye hili soko” alisema Mtanda.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA>>> BONYEZA HAPA KUSOMA ZAIDI
No comments: