Wafungwa kifungo cha nje washiriki zoezi la usafi jijini Mwanza
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Baadhi ya wafungwa wanaotumikia kifungo cha nje, wameshiriki zoezi la kufanya usafi katika soko la Mbugani jijini Mwanza, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani 2024.
Zoezi hilo la usafi limefanyika Jumatano Juni 05, 2024 likihusisha wafungwa 20 wa kifungo cha nje kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa soko la Mbugani pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Akizungumza baada ya kumaliza usafi, Afisa Huduma za Uangalizi Mkoa wa Mwanza kutoka Wizara ya mambo ya Ndani ya Nchi, Magnus Rwekaza alisema wafungwa hao wamekuwa wakishiriki shughuli mbalimbali katika jamii na wanaokoa kiasi kikubwa cha fedha za Serikali ambazo zingetumika kuwalipa watu ujira kwa ajili ya kutekeleza shughuli hizo ikiwemo utunzaji wa mazingira katika maeneo ya umma.
"Tunapowatoa gerezani au mahakamani tunawapanga kwenye taasisi za Serikali kwa ajili ya kufanya usafi, pia kama mfungwa ana taaluma fulani, tunamtafutia sehemu ambayo ataitumia hiyo taaluma yake kama adhabu kwa sababu halipwi na wanafanya kazi kwa muda wa masaa manne kwa siku za kazi baada ya hapo wanarudi kwenye familia zao" alisema Rwekaza akiongeza kuwa kifungo cha nje kinasaidia kupunguza msongamano wa wafunga magerezani.
Pia Rwekaza alieleza kuwa wafungwa hao wapo nje kwa ajili ya kuinufaisha jamii baada ya kuwa wameikosea kwa kujihusisha na matukio ama makosa mbalimbali ambayo ni kinyume cha sheria.
Nao baadhi ya wafungwa wa kifungo cha nje walioshiriki zoezi hilo la usafi, walikiri kujifunza tabia njema wakati wakitumikia kifungo chao na kwamba wamejifunza kuishi na jamii vizuri hususani katika sehemu za umma walizopangiwa kutumikia kifungo chao.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Afisa Huduma za Uangalizi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Magnus Rwekaza (wa kwanza kushoto) akiwa na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza baada ya kushiriki zoezi la usafi katika soko la Mbugani.
Zoezi la usafi likifanyika katika soko la Mbugani jijini Mwanza.
No comments: