Jiji la Mwanza laendelea kutekeleza Mpango Kabambe wa Maendeleo
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wadau mbalimbali wa maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wamekutana na kujadili utekelezaji wa mpango kabambe wa maendeleo (Master Plan) wa Halmashauri hiyo wa mwaka 2015-2035.
Mpango huo ulizinduliwa mwaka 2019 kama dira ya miaka 20 ya kusimamia maendeleo ya Jiji hilo ikiwemo kutoa mwongozo wa kuboresha na kuendeleza matumizi ya ardhi, miundombinu, mawasiliano na uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza Agosti 16, 2024 kwenye kikao cha kujadili mpango huo, Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine alisema lengo ni kufanya mapitio ya utekelezaji wa mpango huo ili kutathimini, kuboresha ustawi na ustahimilivu wa Jiji hilo.
"Mpango huu umejikita katika maboresho na uendelezaji wa miradi mbalimbali katika kuibua uchumi, upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambao utasaidia katika usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi, upanuzi wa uwanja wa ndege, uendelezaji wa makazi yasiyo rasmi mfano maeneo ya Igogo, Pamba na Mabatini" alisema Sima.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Butimba jijini Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji, Marwa Mbusiro aliwaomba wananchi kuachana na ujenzi holela kwani unaweza kuwasababishia hasara na badala yake wafuate sheria na taratibu kwa kufika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ili kupata vibali vya ujenzi.
"Ili Jiji la Mwanza lizidi kupendeza ni lazima tujenge kwa kufuata utaratibu wa ujenzi ambao upo kwenye Mpango Kabambe wa Jiji la Mwanza, kuna watu wachache wanaohujumu mpango huu kwa maslahi yao binafsi kwa kutoa vibali vya ujenzi hata sehemu ambazo hazistahili kuwa makazi ya watu, hivyo wananchi wanatakiwa kuwa makini wanapofuatilia vibali vya ujenzi" alisema Mbusiro.
Naye Afisa Mipango Miji Mwandamizi Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Evodia Paul alisema utekelezaji wa mpango huo umefikia asilimia 35 na kwamba ifikapo mwaka 2035 utakuwa umetekelezeka kwa ukamilifu.
"Huu mpango kabambe unaelekeza kwa kipindi fulani nini kifanyike na endapo tutakuwa na sehemu ambayo hatujaitekeleza huwa tunahuisha ili yale mambo ambayo yanakuwa hayajafanyika yaweze kufanyika, hata sasa tumehuisha mpango wa 2002- 2012 ndio ambao tunaendelea nao na tumeuboresha kutokana na kasi ya ukuaji wa dunia inayohitaji miji ya kisasa zaidi" alisema Evodia.
Wadau wakiwa kwenye kikao hicho.
Wadau wakifuatilia kikao hicho.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
No comments: