Serikali yaahidi kuboresha zaidi Chuo cha Mipango, Mwanza
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeahidi kuendelea kukiboresha Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa kilichopo jijini Mwanza chini ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini ikiwemo kuongeza miundombinu ya kufundishia pamoja na mabweni.
Hayo yameelezwa Jumamosi Agosti 17, 2024 na Mkurugenzi wa Mipango kutoka Wizara ya Fedha, Moses Dulle wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kwenye uzinduzi wa kituo hicho kilichopo eneo la Kisesa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.
"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenielekeza kuzingatia mahitaji ya chuo hiki katika mipango yetu ijayo hivyo kama Wizara ya Fedha niahidi kwamba tutashirikiana na Baraza la Chuo ili kutekeleza mahitaji yaliyoelezwa hapa ikiwemo ujenzi wa miundumbinu ya kufundishia na mabweni" alisema Dulle.
Awali Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya alisema kituo hicho cha Kanda ya Ziwa kilianza kutoa mafunzo mwaka 2011 kwa kutumia majengo ya kupanga na mwaka 2020 uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Magu ulikipatia ardhi hekari 20 katika eneo la Katumba, Kisesa na kuanza mchakato wa ujenzi wa majengo yake.
"Uongozi wa chuo kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Magu ulifanya tathmini na kulipa fidia ya ardhi hekari 60 kwa thamani ya shilingi bilioni 1.7 na hivyo kufanya eneo lote kuwa hekari 80 na kuanza ujenzi wa miradi 17 ya chuo ikiwemo majengo ya taaluma, utawala, maktaba, kitega uchumi, ukumbi wa mikutano, Zahanati, mgahawa na mabweni ambapo hadi kufikia Julai mwaka 2024 jumla ya miradi tisa imetekelezwa ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 14.4" alisema Mayaya.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini alisema tayari mchakato wa mabadiliko ya sheria ya chuo ili kubadili usajili wa Kituo hicho kutoka Kituo cha Mafunzo Kanda kuwa Kampasi kamili na hivyo kuitwa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kampasi ya Mwanza.
Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Magu- Joshua Nasari, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Jubilate Lauwo alisema jitihada za kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka chuo hicho zinaendelea kufanyika ili kwa hiari yao waridhie kuachie maeneo yao kupisha uwekezaji wake kwani mahitaji ya miundombinu ni makubwa kwani idadi ya wanafunzi imeendelea kuongezeka kutoka 323 mwaka 2011/12 hadi 3,845 mwaka 2023/24.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi wa Mipango kutoka Wizara ya Fedha, Moses Dulle akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa kilichopo Kisesa Mwanza chini ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini.
Mkurugenzi wa Mipango kutoka Wizara ya Fedha, Moses Dulle akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Mkurugenzi wa Mipango kutoka Wizara ya Fedha, Moses Dulle akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya
Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilianzishwa mwaka 1979 na mwaka 2011 Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa kilicho chini ya chuo hicho kikaanzishwa jijini Mwanza kwa kutumia majengo ya kupanga hadi mwaka 2020 kilipoanza ujenzi wa majengo yake ambayo yamezinduliwa rasmi Agosti 17, 2024 eneo la Kitumba, Kisesa nje kidogo ya Jiji la Mwanza.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA>>> Bonyeza hapa kusoma zaidi
No comments: