Washiriki Maonesho ya Afrika Mashariki 2024 wapewa rai
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Washiriki wa maonesho ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki wamehimizwa kufuata sheria na taratibu za mauzo wakati wa maonesho hayo kwa kutoa risiti halali wanapouza bidhaa zao.
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kenene alitoa rai hiyo Septemba 04, 2024 wakati akitoa taarifa kwa umma kupitia waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa maonesho hayo.
"Tunawaomba sana wafanyabiashara walipe kipaumbele suala la risiti katika kipindi chote cha maonesho" alisema Kenene.
Alisema idadi ya makampuni yanayoshiriki maonesho hayo ni 235 ambapo 200 ni kutoka ndani ya nchi na 35 ni ya nje ya nchi.
"Makampuni mbalimbali ya binafsi na umma, idara za Serikali na mifuko ya hifadhi za jamii ni miongoni mwa washiriki. Mwaka uliopita maonesho yalitembelewa na watu wapatao 250,000 kutoka Mkoa wa Mwanza na miji inayozunguka Jiji la Mwanza, tunategemea idadi hiyo kuongezeka mwaka huu kufikia watu 300,000" alisema Kenene.
Akizungumzia malengo ya maonesho hayo, Kenene alisema ni kutoa fursa kwa makampuni ya Tanzania na Afrika Mashariki katika kujitangaza, kutumia fursa kwa jumuiya ya wafanyabiashara kuimarisha mtandao wa masoko na usambazaji wa bidhaa zao na makampuni ya Tanzania kujifunza na kupanua wigo wa biashara za nje kwa kutumia fursa zilizopo za makubaliano ya kibiashara kati ya Tanzania na nchi zingine kama EAC, SADC, AGOA na EBA.
Maonesho hayo yalianza Ijumaa Septemba 06, 2024 na yanatarajiwa kufikia tamati Jumapili Septemba 15, 2025 ambapo yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
No comments: