LIVE STREAM ADS

Header Ads

Viongozi Huduma ya Matengenezo ya Kiroho walilia amani kuelekea chaguzi zijazo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Watanzania wametatakiwa kuilinda na kuitunza tunu ya amani waliyopewa na Mwenyezi Mungu ili kuendelea kuwa na Taifa salama hususani katika kipindi cha kuelekea chaguzi.

Rai hiyo imetolewa Jumamosi Oktoba 26, 2024 na Kiongozi wa Huduma ya Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni, Mwl. Augustine Tengwa wakati akizungumza kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Igoma jijini Mwanza. 

Alisema watanzania wanapaswa kujiepusha na viashiria vya uvunjifu wa amani ikiwemo kutengeneza fitina ya kuchafua na kuharibu mwenendo wa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Taifa hili lazima libaki na amani yake kama msingi wake ulivyojengwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere" alisema Mwl.Tengwa

Kwa upande wake Nabii kutoka Huduma ya Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni, Alpha Kihamba alisema Mungu amekuwa akiwaonesha mambo mbalimbali yanayoweza kutokea katika kipindi cha uchaguzi ambapo ametoa wito kwa Serikali na viongozi wa dini kuchukua hatua mapema.

"Kila mmoja kwa dini na dhehebu lake tumuombe Mungu msamaha ili aweze kutuepusha na majanga mbalimbali yakiwemo ya umwagaji wa damu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, mashetani yaliyokusudia kuifanya Tanzania imwage damu hayataweza kwa sababu watumishi wa Mungu tupo na tutaomba sana amani" alisema Kihamba

Naye Mtumishi wa Mungu, Agness Bruno alisema watanzania wasipuuze ujumbe wa manabii hao kwani ni viumbe waliochaguliwa na Mungu kwa ajili ya Taifa Tanzania.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kiongozi wa Huduma ya Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni Mwl.Augustine Tengwa (kulia) akizungumzia suala la kulinda amani kwenye mkutano wake na waandishi wa habari jijini Mwanza. Kushoto ni Nabii Alpha Kihamba.
Nabii Alpha Kihamba (katika) akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha waandishi wa habari na viongozi wa dini, kushoto ni Mtumishi wa Mungu Agness Bruno.

No comments:

Powered by Blogger.