Wafanyakazi TPA Mwanza wajiandikisha daftari la wakazi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambao ni wakazi wa Kata ya Pamba jijini Mwanza, wamejitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wakazi ili kupata sifa ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024.
Watumishi hao wamejiandikisha katika Kituo cha Soko Kuu na kutumia fursa hiyo kutoa rai kwa wananchi na watumishi wa taasisi mbalimbali kujiandikisha kabla ya mwisho wa zoezi hilo, Oktoba 20,204.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Meneja wa TPA Kanda ya Ziwa, Erasto Lugenge (wa pili kushoto waliokaa) akiwa na baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo wakati wa zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wakazi kwa ajili ya kupata sifa ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Baadhi ya watumishi wa TPA Kanda ya Ziwa wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kujiandikisha kwenye daftari la wakazi kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA)Kanda ya ziwa Victoria imewaasa watanzania kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Makazi ili waweze kupata haki ya kuchagua viongozi wanaowataka kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27 Mwaka huu.
Meneja wa Mamlaka hiyo, Erasto Lugenge ametoa wito huo wakati alipowaongoza baadhi ya wafanyakazi wa Tpa wanaoishi kwenye mtaa wa soko kuu kata ya pamba jijini Mwanza katika zoezi la uandikishaji kwenye daftari la makazi la wapiga kura.
"Tumekuja kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa na kama unavyofahamu,Bandari ni sehemu ambayo inaongozwa na uongozi wa serikali za mitaa kwa maana ya kwamba tuna wafanyakazi wanaoishi kwenye serikali za mitaa na vitongoji vyake,abiria wanaosafiri kutumia bandari zetu huwa wanatoka serikali za mitaa lakini tuna wateja na wafanyabiashara wanaotoka serikali za mitaa na zaidi ya hapo miundombinu inayoingia na kutoka bandarini inahudumiwa na Serikali za Mitaa’’alisema Lugenge na kuongeza kuwa;
"Tumeona sisi kama taasisi kuungana na watanzania wenzetu kuja kujiandikisha ili tuweze kuwapigia kura na kupata viongozi makini ambao watatusaidia kusukuma ajenda mbalimbali zinazohusiana na ustawi na maendeleo ya bandari" alisema.
Baadhi ya wafanyakazi wa bandari waliojiandikisha kwenye mtaa wa Soko kuu la mwanza wamesema kuwa zoezi hilo lina umuhimu mkubwa kutokana na kutoa fursa kwa kila mtanzania mwenye sifa kuweza kuchagua kiongozi anayemtaka kwenye ngazi ya Kitongoji, Mtaa na Kijiji.
Wafanyakazi hao Doreen Minja na Francisco Mwanga wamewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Makazi ili wapate haki ya kushiriki na kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika nchini kote.
Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwenye daftari la makazi lilianza nchini Oktoba 11, 2024 na litafikia tamati Oktoba 20, 2024 ambapo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika Movemba 27, 2024.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA>>> Bonyeza hapa kusoma zaidi
No comments: