LIVE STREAM ADS

Header Ads

Madiwani Jiji la Mwanza wakumbushwa wajibu wao

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mstahiki Meya wa Halmshauri ya Jiji la Mwanza, Sima Constantine akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo kilicholenga kujadili taarifa za utekelezaji ngazi ya Kamati kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Na Hellen Mtereko, Mwanza
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wametakiwa kusimamia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao hatua itakayosaidia kuwa na miradi ambayo inakidhi viwango.

Rai hiyo imetolewa Alhamis Novemba 14, 2024 na Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Sima Constantine ambaye pia ni diwani wa Kata ya Mhandu kwenye kikao cha baraza la madiwani kilicholenga kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji ngazi ya kamati kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Sima alisema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo usimamizi wa miradi hiyo unatakiwa ufanyike ili thamani ya fedha iweze kuonekana.

"Shirikianeni na wataalamu katika kusimamia miradi iliyopo na inayoendelea kutekelezwa katika maeneo yenu ili iweze kuwa na tija kwa wananchi" alisema Sima.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba alisema kupitia mapato yao ya ndani wataendelea kutatua changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na madiwani ikiwemo ya upungufu wa vyumba vya madarasa.

"Hadi sasa Halmashauri tumetenga bilioni1.8 kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kwa lengo la kutatua changamoto ya upungufu wa madarasa katika shule za msingi. Pia kutoka Serikali Kuu kupitia mradi wa BOOST tayari zimetoka shilingi milioni 351 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Shadi katika Kata ya Luchelele" alisema Kibamba.

Naye Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Sharifa Mdee aliwapongeza madiwani kwa kuwasilisha changamoto za wananchi katika baraza hilo huku akisisitiza utekelezaji wa ilani kufanyika kwa busara.

Awali diwani wa Kata ya Luchelele, Vicenti Tege alisema shule ya msingi Luchelele ina upungufu wa vyumba vya madarasa 39 na hivyo kuomba changamoto hiyo kutafutiwa ufumbuzi.

Pia alisema bado kuna changamoto ya wanafunzi wa Sekondari kutembea umbali mrefu kutoka Mitaa ya Sweya, Kisoko Malimbe na Silivini kwenda Luchelele Sekondari.

"Watoto hawa wanatembea umbali mrefu sana kwenda kuitafuta elimu hivyo kuna haja ya kujenga shule moya ya Sekondari kwenye maeneo hayo ili kuwapunguzia mwendo" alisema Tege.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba akizungumza kwenye Baraza la madiwani.
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwa kwenye baraza.
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha baraza.

No comments:

Powered by Blogger.