MUHAS kujenga kituo jumuishi cha michezo
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

***
Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Muhimbili ipo katika mpango wa kujenga kituo Jumuishi cha Michezo kwa lengo la kuhimiza ufanyaji mazoezi katika jamii.
Rai hiyo imetolewa Novemba 24,2024 na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Apolinary Kamuhabwa wakati wa kuhitimisha mbio za Reunion Fun Run msimu wa tatu zilizofanyika katika viwanja vya Muhimbili.
‘’Lengo kubwa ni kutafuta rasilimali fedha ili tuweze kujenga kituo cha michezo katika kampasi ya Muhimbili. Wote tunahitaji kituo cha michezo kwajili ya wafanyakazi wa Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ,wanafunzi wa Muhas na wafanyakazi wa chuo hicho, wananchi wa Dar es Salaam na wagonjwa watakaokuwa na nafuu na wenye kuhitaji mazoezi’’ alisema.
Akielezea zaidi kuhusu ujenzi wa kituo cha Michezo, Profesa Kamuhabwa alisema ujenzi wa kituo hicho cha michezo unatarajia kuanza mwakani 2025.
Alisema kituo hicho kitakuwa na uwanja wa mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu pamoja na sehemu ya mazoezi ya viungo (GYM).
Alisema pia kutakuwa na vyumba vya kubadilishia nguo pamoja na vyoo.
Alisema jamii imekuwa inakabiliwa na changamoto ya kutokufanya mazoezi jambo linalopelekea kuongezeka kwa magonjwa yasioambukizwa kama shinikizo la damu na kisukari.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk Ntuli Kapologwe alikipongeza chuo cha Muhas kwa mpango wa kujenga kituo cha michezo.
‘’Serikali tumeungana na Muhas kwajili ya kuhamasisha kampeni ya Mtu ni Afya, huu ni utaratibu mzuri wa kufanya mazoezi sisi kama Wizara ya Afya tumekuwa tukihamasisha vyuo, Idara mbalimbali kuwa na utaratibu mzuri wa kufanya mazoezi’’ alisema.
Dk Ntuli alisema mbio hizi siyo tu zitahamasisha mazoezi, bali pia zinasaidia kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo.
‘’Hii ni sehemu ya kuhamasisha kampeni ya Mtu Ni Afya inayolenga kuhakikisha kila mtu anajali afya yake” alisema Dkt. Kapologwe.
No comments: