LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali ya Rais Samia kupanua Chuo cha MUHAS

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Maendeleo ya nchi yanategemea ubora wa afya za wananchi wake na ili kufikia huko ni lazima nchi iwe na watalaamu wa afya wa kutosha.

Kwa kuzingatia umuhimu wa afya kwa wananchi, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassam imeridhia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kuingia mkataba wa ushirikiano wa shilingi bilioni 50.1 na kampuni mbili za ujenzi wa kujenga Chuo kipya cha Tiba katika kampasi yake ya Mloganzila.

Ujenzi huo utakaofanywa na kampuni ya Mohamed Builders Limited na kampuni ya Kichina ya Hainan International Limited, unajumuisha uendelezaji wa kumbi za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,400, jengo la utawala lenye ofisi za watumiaji 450, maktaba na jengo la TEHAMA linaloweza kubeba watumiaji 550 mara moja.

Awamu ya kwanza ya ujenzo itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 23.4 na itahusisha ujenzi wa jengo la utawala, maktaba, vifaa vya TEHAMA, na miundombinu ya ziada, ikijumuisha uwanja wa mpira na njia za waenda kwa miguu.

Awamu ya pili itakayokuwa na thamani ya shilingi bilioni 26.7 italenga kujenga kumbi za mihadhara, maabara, hosteli za wanafunzi na mikahawa.

Mradi huu ni sehemu ya mpango wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na ni sehemu muhimu ya juhudi za serikali za kuimarisha sekta ya afya nchini Tanzania.

Uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya afya ni kipaumbele kilichoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama tawala cha CCM 2020-2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wa 2021/22-2025/26, na Dira ya Maendeleo 2025.
#KaziInaongea

No comments:

Powered by Blogger.