LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wananchi Babati wamshukuru Rais Samia

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Tujiandae kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Vitongoji na Vijiji Novemba 27,2024.
***

Wananchi wa Babati mkoani Manyara wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea madaraja saba pamoja na kufungua barabara katika kata hiyo ambayo kwa kipindi kirefu wamekuwa wakipata adha ya usafiri hususan kipindi cha mvua.

Akitoa pongezi hizo Diwani wa Kata ya Babati, Haruni Msalu amesema kwamba wanamshukuru Rais kwa kuwatendea haki Kata ya Babati kwani Kata hiyo ilikuwa na makorongo mengi sana na kusababisha wananchi kuteseka hasa kipindi cha mvua na hivyo kusababisha kusimamisha kwa muda shughuli zao za kila siku.

Amesema katika kipindi cha Awamu ya sita Serikali kupitia TARURA imeweza kujenga madaraja yapatayo saba katika Kata ya babati katika eneo la Amboni C, Kambi ya Fisi, Hostel ya Chuo cha Uhasibu na Old Majengo-Angoni.

“Old Majengo kuja Angoni kulikuwa na korongo kubwa ambalo lilikuwa likipitisha maji kwenda ziwani, wananchi wakiwemo wanafunzi walikuwa wakipata tabu sana kuvuka na hivyo kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi kwani iliwapaswa kusitisha kwa muda kupita katika korongo hilo”.

Msalu aliongeza kusema kuwa katika mpango wa TARURA Wilaya ya Babati walitenga fedha kwa ajili ya kujenga madaraja pamoja na kufungua barabara “kwa kweli niwapongeze wafanyakazi wa TARURA kwa kutufungulia barabara kwani wananchi wa Babati Mjini, majengo, Kware na mtaa wa Angoni wamenufaika na ujenzi huu” amesema.

“Kwa bajeti hii ya 2024/2025 tumeendelea kutatua changamoto ambapo daraja la Mnara-Kijiweni sasa hivi ujenzi unakamilika na watu wameanza kupita lakini kazi ya kumwaga changarawe itaanza, niendelee kuwapongeza TARURA kwani katika pindi cha miaka minne kujenga madaraja saba ni kazi kubwa sana na bado wanaendelea kutuhudumia na wananchi tupo na imani na Serikali” amesisitiza.

Hata hivyo diwani huyo amesema wao kama viongozi wa ngazi ya Kata wameendelea kusimamia miradi kwa kushirkiana na wataalam ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma wanazostahili.

Naye Omary Nyange, mkazi wa Mrara alisema wanatoa shukrani nyingi sana kwa Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa madaraja kwani Wilaya ya Babati inapokea mazao mengi kutoka vijijini na biashara za mazao zinafanyika kwa wingi hivyo kukamilika kwa madaraja hivi sasa hakuna changamoto yeyote ya usafirishaji ambapo mazao yanaweza kufika mjini bila shida yeyote.

Aliongeza kwamba kwa kukamilika kwa madaraja hayo hivi sasa wanafunzi wanaweza kuhudhuria vipindi vyote vya masomo kwani hakuna kizuizi chochote katika makorongo hayo kwa sasa.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Babati, Mhandisi Naftari Lyatuu alisema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa madaraja makubwa mawili na madaraja madogo matano pamoja na barabara ya babati-Mtuka (Km. 6) na barabara ya Nakwa (Km. 6) ambazo zinaunganisha Kata tatu, vyuo vya VETA, Uhasibu pamoja na hifadhi ya taifa ya Tarangire kupitia geti la Mamile kumewezesha kufungua shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi ikiwemo shughuli za kitalii kwani wakazi wengi wanaishi upande huo yalipojengwa madaraja hayo, hivyo kuweza kuwaunganisha na Makao Makuu ya Mji wa Babati.
#KaziInaongea

No comments:

Powered by Blogger.