Kamati ya Fedha na Mipango Jiji la Mwanza yakagua miradi ya maendeleo
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwonekano wa baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kanyerere.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo huku ikisisitiza uadilifu katika matumizi ya fedha za Serikali.
Kamati hiyo ikiongozwa na Naibu Mstahiki Meya, Bhiku Kotecha imefanya ziara hiyo Jumatatu Novemba 04, 2024 na kukagua miradi mitatu ikiwemo Zahanati ya Mhandu, Shule ya Msingi Kanyerere na Shule ya msingi Shadi iliyopo Kata ya Luchelele.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kotecha alisema miradi hiyo itakapokamilika wananchi watapata huduma bora za elimu na afya.
"Miradi hii inaendelea vizuri na wanaosimamia miradi hiyo wahakikishe wanasimamia vizuri ili thamani ya fedha iweze kuonekana pia tumesisitiza ikamililike kwa wakati ili wananchi wa maeneo haya waweze kupata huduma za elimu na afya karibu" alisema Kotecha.
Naye mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Charles Nyamasiriri alisema miradi waliyoitembelea hakuna yenye changamoto hivyo ameiomba Halmashauri kuendelea kupeleka fedha kwa wakati ili miradi iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Tambukareli anayesimamia ujenzi wa shule ya msingi Kanyerere, Mniko Emmanuel alisema ujenzi wa shule hiyo utakapokamilika utasaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika shule yake ambayo ina wanafunzi 3,245.
"Shule hii itakapokamilika itakuwa na madarasa 13, hadi sasa yaliyokamilika ni matano na itapunguza msongamano katika shule ya msingi Tambukareli kwani itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,500" alisema Mwl. Mniko.
No comments: