LIVE STREAM ADS

Header Ads

Madaktari bingwa zaidi ya 60 wa Rais Samia wapiga kambi Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Madaktari bingwa na bobezi zaidi ya 60 wameweka kambi jijini Mwanza kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za kimatibabu kwa wananchi na kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili kuendelea kutoa huduma zilizo bora.

Hayo yamebainishwa Jumatatu Novemba 04, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa Mwanza, Elikana Balandya wakati akizindua huduma za kibingwa na bingwa bobezi awamu ya pili katika Hospitali za Halmashauri zitakazofanywa na madaktari wa Rais Dkt.Samia Suluhu kuanzia Novemba 04 hadi 09,2024.

Balandya alisema huduma ambazo zitatolewa na madaktari hao ni magonjwa ya wanawake na ukunga, magonjwa ya watoto na watoto wachanga, huduma ya upasuaji na upasuaji wa mfumo wa mkojo, magonjwa ya ndani, huduma ya kinywa na meno na upasuaji wa mifupa.

Alisema wananchi wa Mkoa huo wenye matatizo ya kiafya wanapaswa kuhudhuria katika hospital zao ili waweze kupata matibabu kutoka kwa kadaktari bingwa na bingwa bobezi katika kambi walizopiga ambapo itawasaidia kuepuka gharama za usafiri, kusafiri umbali mrefu na baadhi ya wagonjwa kutoka nje ya Wilaya na Mkoa.

Balandya alieleza kuwa huduma hizo zitatolewa katika hospital tisa zenye hadhi ya Wilaya ambazo ziko katika Halmashauri nane za Mkoa wa Mwanza ambazo ni Ilemela, Nyamagana, Buchosa, Kwimba, Misungwi, Magu, Sengerema, Nansio na Bwisya.

"Huduma hizi zimesogezwa kwetu inabidi na sisi wananchi wa Mkoa wa Mwanza tuzitumie vyema kwani huwa ni mara chache sana huduma hizi za kibingwa na bingwa bobezi kuzipata katika maeneo yetu" alisema Balandya.

Alisema huduma hizo zinahitajika ili kuendelea kuboresha afya ya wananchi wa Mkoa huo ukizingatia wamekuwa wakipokea wagonjwa wengi wa nje kwa ajili ya matibabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya ya Mtoto, Mtoto mchanga na Vijana kutoka Wizara ya Afya, Felix Bundala alisema tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo ya matibabu bungwa, tayari wametoa huduma katika mikoa 20, Halmashauri 137, Vituo 139 na kuwafikia wagonjwa elfu 60.

Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospital ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Timothy Kibina alieleza kuwa utoaji wa huduma hiyo umewasaidia wananchi wengi kutokana na hospitali zinazotoa huduma za kibingwa kuwa mbali na mazingira wanayoishi.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elkana Balandya akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma za kibingwa na bingwa bobezi awamu ya pili katika Hospitali za Halmashauri za Mkoa wa Mwanza zitakazofanywa na madaktari wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya ya Mtoto, Mtoto Mchanga na Vijana- Felix Bundala akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma za kibingwa na bingwa bobezi awamu ya pili katika Hospitali za Halmashauri za Mkoa wa Mwanza.
Baadhi ya madaktari wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan wakiwa kwenye kikao cha uzinduzi wa huduma za kibingwa na bingwa bobezi awamu ya pili katika Hospital za Halmashauri za Mkoa wa Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.