LIVE STREAM ADS

Header Ads

SAMIA: Misingi ya uongozi imenisaidia kukabiliana na changamoto

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza namna misingi ya uongozi wake katika kufanya maamuzi ilivyoiwezesha Serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi ndani ya miaka mitatu ya Awamu ya Sita, ikiwemo athari za mlipuko wa UVIKO-19 na migogoro ya kimataifa ambayo iliathiri mwenendo wa uchumi wa dunia.

Rais Samia amesema, misingi inayoshajihisha uongozi wake ni ufanyaji wa maamuzi kwa kushirikisha wadau, kwa kuongozwa na ushahidi na utafiti na kwa kutanguliza mbele maslahi ya Taifa na watanzania.

Aliyasema hayo wakati akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Uongozi na Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Morogoro, kwenye mahafali ya 23 ya Chuo hicho.

Itakumbukwa kuwa, Rais Samia alisoma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 1983 hadi 1986, na sasa amekuwa Mtunukiwa wa kwanza wa heshima hiyo katika Chuo hicho.

Ametumia fursa hiyo pia kutambua na kupongeza michango ya Awamu za Uongozi zilizotangulia iliyoliwezesha Taifa kuwa lenye Utawala bora, utulivu wa kisiasa, uchumi imara, amani na mshikamano.

Pamoja na yote pia amesisitiza kuwa, kiongozi ni mtumishi anayeendeleza ya jana, anayebuni, kuibua na kutekeleza ya leo na anayeacha ya kuendelezwa kwa ajili ya kesho na ametoa rai kwa viongozi wote kwa nafasi zao, kufanya kazi na kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia maadili na uadilifu.

Akizungumzia elimu ya juu, Rais Samia amesema Serikali itaongeza uwekezaji katika Teknolojia, tafiti zenye manufaa na mipango kwa lengo la kuimarisha elimu ya juu na kuwezesha wahitimu kuwa na ushindano kikanda na kimataifa.

Amerejea rai yake kwa Vyuo Vikuu nchini, kujielekeza katika kujibu changamoto za mazingira ya sasa, Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
#KaziInaongea

No comments:

Powered by Blogger.