Hospitali ya JKCI, Benki ya CRDB zaunganisha nguvu sekta ya afya
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutaka kumpunguzia mwananchi gharama za matibabu zimeendelea kuzaa matunda, ambapo sasa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeungana na benki ya CRDB katika kumpunguzia gharama za matibabu mteja wa benki hiyo sanjari na watoto.
CRDB na JKCI zimedhamiria kushirikiana katika kuchangia huduma ya matibabu na vipimo kwa watoto na wateja wa benki hiyo.
Benki hiyo imeweka punguzo la asilimia 50 kwa wateja wake wanaopitishia mishahara yao kwao na kwamba watapata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa gharama nafuu.
Akizungumzia ushirikiano huo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa ushirikiano na CRDB amesisitiza kuwa wataendelea kutoa huduma kwa jamii.
CRDB imekuwa ni mshirika muhimu kwenye sekta ya afya kwani tangu mwaka 2017 benki hiyo imechangia kiasi cha Shilingi Milioni 775 zilizotumika kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto 193.
Kwa upande wake mwakilishi wa CRDB, Bruce Mwile amesema, makubaliano waliyoingia na JKCI ni mwanzo wa ushirikiano utakaoleta manufaa kwa wengi katika maeneo ya huduma za matibabu ya moyo kwa kuwawezesha wateja wa CRDB kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
#KaziInaongea
No comments: