Stars yamfuta machozi Rais Samia, watanzania
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imfuta machozi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na watanzania kwa ujumla kutokana na ajali ya kuanguka kwa ghorofa, Kariakoo jijini Dar es Salaam baada ya kuipeleka Tanzania AFCON 2025 nchini Morocco.
Stars imelifanya hilo Novemba 19,2024 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, ambapo imefuzu kucheza fainali za AFCON 2025 zitakazochezwa nchini Morocco kwa kuichapa timu ya Taifa ya Guinea bao 1-0.
Stars ilihitaji ushindi wa aina yeyote kwenye mchezo huo ili kusonga mbele na ndicho ilichokifanya mbele ya Watanzania wengi ambao wamegubikwa na majonzi ya kupoteza Watanzania wenzao kwenye ajali ya kuanguka kwa ghorofa.
Vitambaa vyeusi kwenye mikono ya wachezaji wa Taifa Stars vikiashiria majonzi vilitosha kuwapa ari na nguvu wachezaji kuwafariji Watanzania wenzao.
Kama hiyo haitoshi Rais Samia ambae amekuwa kinara wa kufanikisha mafanikio ya Stars aliamua kununua tiketi zote za mchezo huo ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengi kushuhudia mchezo huo na baada ya ushindi huo Rais Samia amewazawadia shilingi milioni 700 kama pongezi kwa kufuzu kwenda
AFCON 2025.
Mbali na hayo Rais Samia pia amekuwa mstari wa mbele katika kununua magoli ya ushindi, akichagiza kampeni yake ya 'Bao la Mama'.
Ni Simon Msuva ndie aliyerejesha furaha kwa Watanzania baada ya kufunga bao zuri la kichwa.
Akizungumza baada ya mchezo kumalizika kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman Morocco, amemshukuru Rais Samia na Watanzania kwa ujumla kutokana na sapoti yao kwa timu.
Shukurani hizo pia zimetolewa na Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta ambae amesema uamuzi wa Rais Samia wa kuruhusu watu kuingia bila kulipa kiingilio umesaidia kuwaongezea hamasa.
Pongezi zaidi kwa benchi la ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na Kocha Hemed Suleiman Morocco akisaidiwa na Juma Mgunda na Jamhuri Kihwelu 'Julio'.
#KaziInaongea
No comments: