Serikali yajizatiti mapambano dhidi ya a VVU
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zimezaa matunda, baada Mkoa wa Ruvuma kutajwa kuwa kinara kwa watu kujitokeza kupima virusi vya ukimwi na utumiaji dawa wa kudhoofisha virusi vya ugonjwa huo.
Hayo yamebainika wakati Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed akifungua wiki ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo Kitaifa yanafanyika Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa amesema, wananchi wa Mkoa huo wametajwa kuwa mstari wa mbele kujitokeza kupima Virusi vya Ukimwi pamoja na kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo kwa wagonjwa waliobainika kupata maambukizi ya virusi hivyo.
Taarifa hizo pia zimeeleza kuwa, Mkoa huo umefanikiwa kupunguza maambukizi ya HIV ambapo maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 0.7 kutoka asilimia 5.6 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 4.9 mwaka 2022.
Mkoa wa Ruvuma umeendelea kufanya vizuri katika viwango vya “95 95 95” ambapo utafiti wa mwaka 2023 unaonyesha asilimia 82 za wananchi wa Mkoa huo wanatambua hali zao za maambukizi na asilimia 97 wanatumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI na asilimia 90 ya wanaotumia dawa wameshafubaza virusi hivyo.
Kanali Abbas amesema Mkoa wa Ruvuma una jumla ya watu 68,237 wanaoishi na VVU ambapo wanaume ni 24,959 sawa na asilimia 37 na wanawake ni 43,000 sawa na asilimia 63 huku watoto chini ya miaka 15 ni 2382 sawa na asilimia 3.5.
"Halmashauri zinazoongoza ni Manispaa ya Songea ikifuatiwa na Tunduru na Mbinga hivyo nawasihii watu wanao ishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) wote kuzingatia tiba na matunzo ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kufubaza virusi ikiwa ndiyo njia pekee ya kukabiliana na ugonjwa huu" amesema Kanali Abbas.
Mkuu wa Programu kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim, ameupongeza Mkoa wa Ruvuma kwa mapambano ya kushusha kiwango cha maambukizi ikiwa ni pamoja na kuongoza kwa upimaji wa virusi vya UKIMWI kitaifa.
Wiki ya Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yanafanyika katika Mikoa mbalimbali nchini ambapo Kitaifa yanafanyika Mkoani Ruvuma na yanatarajiwa kufungwa Desemba, 1, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Mpango.
#KaziInaongea
No comments: