LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wachimbaji wadogo kupatiwa maeneo ya kuchimba

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati ya kuwapatia Wachimbaji Wadogo maeneo ya uchimbaji na kusaidia kufanya utafiti kwa bei ndogo yenye ruzuku ya Serikali kupitia Shirika la Madini Taifa (STAMICO) na kuratibu mikopo nafuu kufuatia majadiliano mazuri na taasisi za kifedha na mabenki.

Mkakati huu umewekwa kwa lengo la kuwainua wachimbaji wadogo wa madini na kuwaondoa kwenye hujuma za kujiingiza kwenye utoroshaji madini nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema, Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali Wachimbaji wote na wafanyabiashara wa madini ambao hawatafuata Sheria ya Madini na kujiingiza kwenye utoroshaji wa madini, ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni, kutaifisha mali zao na kutoruhusiwa kufanya tena biashara ya madini hapa nchini.

Dkt. Kiruswa amewataka Wachimbaji Wadogo nchini kuchangamkia fursa hiyo ya kufanyiwa utafiti wa uchorongaji na STAMICO kwa bei nafuu yenye ruzuku ya Serikali na kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kujenga na sio kulumbana na kujadiliana mambo ya msingi kwa kuwa shirikisho hilo ni la kibiashara na matarajio ya Serikali ni kuona FEMATA inapiga hatua kubwa huku wanachama wakizika tofauti zao.

Akiongea katika mkutano wa viongozi na Kamati Tendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) Jijini Dar es Salaam amesema, kupitia uongozi mpya wa FEMATA, Serikali inatamani kuona kasoro ya utoroshaji wa madini kwa wachimbaji wadogo inakwisha,
na kuelimisha umuhimu wa ulipaji kodi kwa wachimbaji wadogo wanaowaongoza ili Serikali iweze kutekeleza ipasavyo miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii ambayo inatagemea kwa kiasi kikubwa makusanyo ya ndani kutokana na shughuli mbalimbali za uchumi ikiwa ni pamoja na shughuli za madini.

Amesema, Serikali isingependa kuona uwepo wa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara ambao siyo waaminifu, kwamba, haitosita kuwachukulia hatua kali wachimbaji wote na wafanyabiashara wa madini ambao hawatafuata Sheria ya Madini ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni na kutaifisha mali zao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahaya amesema kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yote ya wachimbaji ili kufanya shughuli zao za uchimbaji kwa tija ikiwa ni pamoja na kuwapatia maeneo ya kuchimba pamoja na kuratibu mikopo nafuu kufuatia majadiliano mazuri na taasisi za kifedha na mabenki.

Naye Rais wa FEMATA John Bina amesema kuwa Mkutano huo wa FEMATA umelenga kuwasaidia viongozi wa Shirikisho hilo ili waweze kutimiza wajibu wao kwa ufanisi zaidi na hatimaye kuleta matokeo chanya huku akimhakikishia Naibu Waziri Dkt. Kiruswa kuwa Shirikisho hilo litaendelea na kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kutumia masoko na vituo vya ununuzi vya madini kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini ikiwa ni pamoja na mazingira bora kwa wachimbaji wadogo.
#KaziInaongea

No comments:

Powered by Blogger.