Rais Samia apongezwa kuboresha mazingira ya biashara
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya biashara nchini, ambapo pia ameikaribisha Jumuiya ya Wafanyabiashara kutoka Nchini Finland kuwekeza kwenye sekta ya madini.
Alisema Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali za kutosha za madini, mazingira ya uwekezaji rafiki na sera zinazotabirika.
Waziri Mavunde aliyasema hayo Novemba 20,2024 Masaki jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kifungua kinywa ulioandaliwa na Ubalozi wa Finland nchini kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara wa Madini kutoka Finland na Wizara ya Madini ili kubaini maeneo ya ushirikiano na fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta ya madini nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting alisema Tanzania na Finland ni nchi zenye ushirikiano mkubwa kwenye masuala ya kiuchumi na hivyo ni wakati muafaka sasa kuimarisha mahusiano hayo kupitia uwekezaji kwenye sekta ya madini ambapo amepongeza hatua kubwa zinazochukuliwa na Rais Dkt. Samia katika kukuza sekta ya madini nchini na kuifanya kuwa sekta muhimu kwenye kuchangia maendeleo ya uchumi ya Tanzania.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Madini ya Finland (GTK), Prof. Tiilikainen Kimmo alisema kwamba kupitia makubaliano (MoU) kati ya GTK na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), Finland itashirikiana na Serikali ya Tanzania kuimarisha shughuli za Utafiti wa madini ili kuiwezesha Tanzania kufikia Dira ya 2030 ya Madini ni 𝐌𝐀𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐧𝐚 𝐔𝐓𝐀𝐉𝐈𝐑𝐈 ambapo Tanzania imejipanga kufanya utafiti wa kina wa madini wa kufikia asilikia 50 ya eneo la nchi nzima.
Akiwasilisha hotuba yake Mavunde aliwakaribisha wafanyabiashara kutoka Finland kuja kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa Tanzania ina fursa nyingi za kiuchumi kupitia sekta ya madini na hasa madini mkakati ambayo kwa sasa yana uhitaji mkubwa duniani.
“Rais Dkt. Samia S. Hassan kupitia Falsafa yake ya uongozi wa 4R ameweka mazingira rafiki ya biashara na uwezekaji nchini Tanzania na hivyo Tanzania ni sehemu salama ya kufanya uwekezaji" alisema.
Tanzania imejaaliwa rasilimali madini ya kutosha na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa na nafasi nzuri kuvutia uwekezaji.
Hivyo tunafungua milango kwa wafanyabiashara kutoka nchini Finland kuchangamkia fursa za uwekezaji kupitia sekta ya madini“ amesema Mavunde.
Wafanyabiashara hao wapo nchini kuhudhuria mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji 2024 unaofanyika nchini Tanzania.
#KaziInaongea
No comments: