Serikali ya Rais Samia yasisitiza maslahi kwa mabondia
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepiga simu moja kwa moja wakati wa tukio maalum la pambano la ngumi la ‘Knockout ya Mama’ lililofanyika katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, Rais Samia amewataka mabondia watanzania kuibeba na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika mchezo wa ndondi.
Kwenye tukio hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi aliiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwawezesha mabondia kunufaika na vipaji vyao.
Ametoa wito huo Disemba 26, 2024 wakati wa pambano la ngumi la ‘Knockout ya Mama’.
“Awali michezo hii ilikuwa ni ridhaa, lakini kwa sasa tumeweka sheria ambazo zinataka mchezo huu uwe wa kulipwa, ambapo mchezaji akiitwa na kuweka mikataba ni lazima apate maslahi”.
Waziri Mkuu ameitaka Wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wa mchezo wa ngumi kuendelea kuhakikisha wanatoa mafunzo bora kwa makocha na wachezaji.
“Hii itawezesha kuwa na uhakika kwamba mabondia wa Kitanzania wanapata ujuzi wa kisasa na wanaendelea kufanya vizuri zaidi”.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameitaka Wizara hiyo kushirikiana na wadau wa mchezo wa ngumi, wahakikishe wanawake wanapatiwa fursa zaidi ili waweze kushiriki na kuonesha vipaji vyao kwenye mchezo wa ngumi.
Amesema Sekta ya michezo imefanyiwa maboresho makubwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali
Akizungumza kuhusu tukio hilo la Knockout ya Mama, Majaliwa amesema kufanyika kwa tukio hilo kunatokana na kazi kubwa na ushirikiano wa wadau mbalimbali wenye nia ya kusaidia maendeleo ya jamii hasa mchezo wa ngumi.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi amempongeza Rais Dkt. Samia kwa mchango mkubwa ambao ameendelea kuutoa katika sekta ya michezo.
“Utashi mkubwa wa Kisiasa wa Mheshimiwa Rais umeleta msukumo chanya na kuongeza ari na kuchochea ukuaji wa sekta hii”.
Katika tukio hilo Rais, Dkt. Samia alipiga simu na kuzungumza na Wadau na mashabiki wa mchezo wa ngumi na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuweka mikakati ya kukuza sekta hiyo.
“najua wapo mabondia wa nje, sasa watanzania ibebeni bendera ya Tanzania” amesema.
KAZI INAONGEA
No comments: