LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watakaobainika kuchelewesha mradi Mwanza kuchukuliwa hatua

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza kumpeleka Mkaguzi wa ndani wa Mkoa kukagua mwenendo wa utekelezaji wa ujenzi wa jengo la wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe.

Hatua hiyo imekuja kufuatia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia, kuwataka watumushi wa Serikali kusimamia sekta ya afya, kutokana na jitihada za Rais kuwekeza nguvu nyingi katika kuboresha mazingira katika Sekta hiyo muhimu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda mapema Ijumaa Disemba 27, 2024 alipotembelea hospitalini hapo, kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la wazazi na kubaini kuna ucheleweshaji wa miezi sita, kinyume na mkataba na kuagiza, ujenzi huo ukamilike ndani ya siku 20.

“Serikali imeleta milioni 900 kwenye hospitali hii kwa ajili ya kujenga wodi muhimu ya wazazi ili kuboresha huduma bora za afya kwa wananchi na kuboresha hali ya utoaji huduma hivyo wasimamizi hampaswi kukwamisha juhudi hizi” amesema Mtanda.

Ameongeza kuwa inashangaza kuona fedha zimeshafika tangu mwezi Machi, 2024 na walipaswa kukamilisha ujenzi mwezi Juni lakini ni Milioni 700 pekee zimelipwa kwa mafundi ikiwa ni asilimia 85 ya fedha zote na kusababisha kuchelewesha ujenzi huo.

Aidha ameelekeza mzabuni wa milango kwenye hospitali hiyo ahakikishe anakabidhi mara moja ili iweze kuwekwa na kukamilisha ujenzi na kuhusu majengo yaliyoandaliwa kufanya upanuzi, ameahidi kuwasiliana na Wizara ili kuhakikisha fedha zinaletwa kukamilisha ujenzi.
KAZI INAONGEA

No comments:

Powered by Blogger.