LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali yapandisha thamani ya korosho

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupandisha bei ya korosho ni miongoni mwa ahadi ahadi zenye manufaa kwa wananchi.

Katika ahadi zake, Rais Samia amesisitiza Serikali yake kuboresha maisha ya wakulima kwa kuhakikisha wanapata bei nzuri ya mazao yao na kuongeza ununuzi wa zao hilo lililofikia tani 401,000 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.44 kwa mwaka 2024/2025.

Mafanikio ya kupandishwa kwa bei ya zao hili, yameongeza thamani kwa mkulima na kupandisha uchumi wa Taifa, ambapo wakati msimu wa ununuzi wa korosho kwa mwaka 2024/2025 ukikaribia kumalizika, mpaka sasa kiasi hicho cha tani hizo za korosho zimenunuliwa.

Katika mnada wa 10 wa chama Kikuu cha Ushirika cha RUNALI kwa msimu wa 2024/2025 uliofanyika Mjini Nachingwea, Afisa Usimamizi wa Fedha Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Prince Mng'ong'o amesema hadi sasa kiasi hicho cha tani za korosho ghafi za Tril.1.44 zimeuzwa na kununuliwa.

Mng'ongo amesema hadi sasa chama Kikuu cha RUNALI kimefanikiwa kuuza tani 70,360 kati ya tani hizo 401,000 zilizozalishwa na Mikoa yote mitano inayolima zao hilo kwa wingi hapa nchini.

Mbali na korosho taasisi hiyo imesimamia mauzo kupitia minada ya zao la kakao ambapo hadi sasa takribani tani 11,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 210 zimeuzwa na kununuliwa.

"Lakini pia TMX imeendesha minada ya madini, mpaka sasa zimeuzwa gramu 610,000 ambazo sawa na kilo 610 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 610 kwa njia ya soko la bidhaa Tanzania, mkakati ni kwamba ifikapo mwaka 2025 mazao yote ya kimkakati yauzwe kwa mfumo wa TMX" amebainisha Mng'ong'o.

Chama kikuu cha RUNALI kilichopo mkoani Lindi kinatarajia kufanya mnada mmoja wa mwisho, ambapo baadhi ya Vyama Vikuu vya Ushirika tayari vimefunga msimu wa ununuzi kwa mwaka 2024/2025.

Katika mnada wa kwanza wa mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara, Oktoba 11, 2024, Rais Samia alipandisha bei ya korosho na kuuzwa kwa bei ya juu ya shilingi 4,120 kwa kilogramu, huku bei ya chini ikiwa Shilingi 4,035.

Kupandishwa kwa bei hii ni historia iliyoandikwa katika mikoa hiyo baada ya mnada huo ulioandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU) ambapo katika mnada huo, jumla ya tani 3,857 za korosho zimeuzwa ambapo kwa wakulima hao, ni mafanikio makubwa ambayo waliyasubiri kwa muda mrefu.

Meneja wa TANECU, Mohamedi Mwinguku ameipongeza Serikali kwa ushirikiano wake na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa wakulima wanafaidika na mazao yao.

Mkurugenzi wa mafunzo na utafiti Wizara ya kilimo, Dkt.Wilheza Mafuru wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa zao la korosho katika siku ya ulaji na unywaji wa zao la korosho katika maonesho ya 88 Nzuguni jijini Dodoma amesema, uwepo wa viwanda utaongeza ajira na pato la mkulima na Taifa kwa ujumla,mahitaji ya korosho ghafi viwandani yatachochea ongezeko la uzalishaji wa korosho na hatimaye kufikia malengo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuzalisha tani 700,000 ifikapo mwaka 2024/25 ukilinganisha na tani 310,000 za msimu wa 2023/24.

"Ulaji wa korosho na bidhaa zake utakuza ubanguaji wa ndani na hivyo kufikia asilimia 60 ya ubanguaji ifikapo mwaka 2024/25 tofauti na ubanguaji wa chini ya asilimia 20 uliopo hivi sasa, ikumbukwe kuwa kati ya korosho zinazozalishwa ni asilimia 10 mpka 20 tu hubanguliwa hapa nchini, wakati asilimia 80-90 husafirishwa nje na wafanyabiashara kama korosho ghafi.
KAZI INAONGEA

No comments:

Powered by Blogger.