Kampeni ya Saratani Kitaa kufanyika Mwanza
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwenyekiti wa Babuu Cancer Foundation- BCF, Cedou Mandingo maarufu kama Babuu wa Kitaa (katikati) akizungumzia kampeni ya Saratani Kitaa inayotarajia kufanyika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
***
Taasisi ya Saratani ya Babuu (Babuu Cancer Foundation- BCF) yenye makao yake makuu jijini Dar es salaam, inatarajia kuendesha kampeni ya Saratani Kitaa katika Jiji la Mwanza kwa lengo la kutoa elimu ya kuhusu ugonjwa huo.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Cedou Mandingo maarufu kama Babuu wa Kitaa ambaye aliwahi kuugua na kupona ugonjwa wa saratani, amesema kampeni hiyo itaambatana na matembezi ya furaha ya kilomita tano katika mitaa ya Jiji la Mwanza ambapo yataanzia na kumalizikia uwanja wa Nyamagana.
Mandingo amesema kampeni hiyo inaanzia katika Jiji la Mwanza baada ya takwimu kuonyesha wagonjwa wengi wanatoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na kwamba itaendelea katika mikoa mingine nchini kwani bado wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo.
Pia ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan kwa jitihada kubwa za kuboresha upatikanaji wa vifaa na matibabu ya saratani ambapo kampeni hiyo ya Saratani Kitaani itatoa fursa kwa wananchi kufahamu mafanikio katika sekta ya afya chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba taasisi ya BCF, Dkt. Frank Rutachunzibwa ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Saratani amesema bado wananchi wengi wana dhana potofu kuhusu ugonjwa wa saratani ambapo badala ya kuwahi hospitalini wao huenda kwenye tiba asili.
Amesema hatua hiyo imesababisha idadi ya vifo kufikia zaidi ya elfu 29 huku wagonjwa wanaobainika wakiwa zaidi ya elfu 44 hiyo ikiwa ni kwa takwimu za mwaka 2022 kutoka Wizara ya Afya hivyo ni vyema wananchi wa Mwanza wakajitokeza uwanja wa Nyamagana ili kupata elimu kuhusu ugonjwa huo.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA>>> Bonyeza hapa kusoma zaidi
No comments: