Simiyu yatakiwa kuachana na mila potofu kupambana na Kipindupindu
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi (katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt Ntuli Kapologwe (wa kwanza kulia) wakiwa kwenye matembezi ya amani katika huo. Wa pili kulia ni balozi wa kampeni ya Mtu Ni Afya, Mrisho Mpoto.
***
Wakazi wa Mkoa wa Simiyu wametakiwa kuachana na mila potofu katika mapambano ya ugonjwa kipindupindu ambapo kwa sasa ugonjwa huo wa mlipuko umekuwa ukisumbua katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo.
Rai hiyo imetolewa Jumatatu Disemba 23, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi wakati wa maombi malumu na matembezi ya upendo wa kuombea mkoa huo pamoja na Taifa kwa ujumla.
Amesema baadhi ya mila zinazoleta changamoto ni kama mila potofu ya baba mkwe na mama mkwe kutumia choo cha pamoja.
Akielezea zaidi, Kihongosi amesema wananchi wa mkoa huo waachane na dhana kuwa maji maji yaliotibiwa na Wakala wa Usambazaji wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) hayafai kwa matumizi.
‘’Maji yaliotibiwa na RUWASA ni mazuri na yamewekewa dawa zilizopitishwa na watalaam wetu kutoka Wizara ya Afya’’ amesema.
Kihongosi amewataka pia wakazi hao wa Mkoa wa Simiyu kuachana na dhana kuwa maji yaliotibiwa yanapunguza nguvu za kiume na kuleta madhara katika kizazi.
‘’Naishukuru Wizara ya Afya ya kuleta kampeni ya Mtu Ni Afya katika kuweza kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa kipindupindu katika mkoa wetu. Tunatambua mkoa wetu unachangamoto ya kipindupindu, awali tulikuwa na idadi kubwa sana ya watu waliopata maambukizi ya ugonjwa huu’’ amesema.
Katika hatua nyingine, Kihongosi amewataka wakazi wa mkoa wa Simiyu kuchemsha maji pamoja kuwa na matumizi ya vyoo bora.
"Tumetembelea Kata zote 133 ndani ya Mkoa huu na kutoa elimu kwa wananchi na kuelezea madhara ya kipindupindu na jitihada hizo zimesaidia kupunguza madhara ya kipindupindu’’ amesema.
Kwa upande wake balozi wa kampeni ya Mtu Ni Afya, Mrisho Mpoto amesema timu ya Mtu Ni Afya itafanya kweli katika kuhakikisha ugonjwa wa Kipindupindu unapinduka kabla ya mwaka 2024 haujaisha.
Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt Ntuli Kapolgwe (katikati) akiwa na wakazi wa mkoa wa Simiyu wakati wa matembezi ya amani.
No comments: