LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali ya Rais Samia yazindua mradi wa kusafirisha umeme, Chalinze- Dodoma

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mafanikio ya utekelezaji wa Miradi mikubwa ya maendeleo katika Serikali ya Awamu ya Sita ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yameonekana dhahiri baada ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko kuzindua utekelezaji wa Mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya kilovoti 400 Chalinze Mkoa wa Pwani na Zuzu mkoani Dodoma.

Mradi huo wa umeme uliozinduliwa utawezesha umeme wote unaozalishwa katika Mradi wa kuzalisha umeme wa JNHPP kufika katika maeneo yote ya mikoa iliyopo Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Migodi, Viwanda na kuimarisha biashara ya umeme Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Dkt. Biteko amesema kutekelezwa kwa Mradi huo, kunatokana na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali pamoja na miongozo yake ya namna bora ya kutekeleza miradi ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika kwa lengo la kukidhi mahitaji ambayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kutokana na jitihada hizo zinazofanywa na Rais Samia katika kuendeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme imepelekea Tanzania kuwa kinara Barani Afrika, katika usambazaji wa umeme kwa wananchi na hii ni kutokana na takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia.

Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na jitihada za kuimarisha upatikanaji wa Nishati ya umeme nchini ambazo zimewezesha kuongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyopo nchini hadi kufikia Megawati 3,169.26 ambapo mahitaji ya juu ya umeme nchini kwa sasa yamefikia Megawati 1,888.72.

Amesema, mahitaji hayo hayajawahi kufikiwa kutoka nchi ipate Uhuru na hii ikimaanisha kuwa uchumi unazidi kukua kutokana na kuongezeka kwa shughuli za maendeleo.

“Kuimarika kwa uzalishaji wa umeme nchini kumechangiwa na kuanza uzalishaji katika Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 99.6 na jumla ya Megawati 1,175 za umeme zinazalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa” amesema Dkt.Biteko.
Dkt.Biteko amekemea vikali wahujumu wa miundombinu ya umeme ambao amesema kuwa, wanarudisha nyuma uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuwafikishia wananchi Nishati ya uhakika na kuagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua kali kwa wahujumu hao ambao wamekuwa wakikosesha wananchi umeme pale miundombinu inapoharibiwa.

Kuhusu Wakandarasi wa mradi huo, Kampuni ya TBEA kutoka China, amewataka wahakikishe mradi unakamilika kwa wakati ili wananchi wapate manufaa yaliyokusudiwa ikiwa pia ni maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt.Biteko ametumia hafla hiyo kuwakumbusha viongozi na wananchi kuhusu jitihada za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutimiza lengo la Serikali la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Katika muendelezo wa jitihada hizo, amesema Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu gharama ya bei ya soko ambapo mitungi hiyo inasambazwa katika Mikoa yote Tanzania Bara.

Ametoa wito kwa Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kwa kutumia majiko ya gesi na teknolojia mbalimbali kulingana na mazingira ikiwemo nishati ya umeme kwani nishati hizi ni miongoni mwa nishati safi, salama na ya gharama nafuu ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
#KAZIINAONGEA

No comments:

Powered by Blogger.