Serikali yaridhishwa na ujenzi wa Kituo cha Kusindika Gesi Asilimia (CNG)
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kukamilisha Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kushindilia Gesi asilia kwenye magari, (CNG) kilichopo Ubungo Jijini Dar es Salaam, ambacho kitaanza kutoa huduma ya kujaza gesi kwenye magari, kuanzia 03, Februari, 2025.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, amefanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo hicho 09, Januari, 2025 Ubungo Jijini Dar es Salaam, ambapo ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kueleza kwamba, kukamilika kwa kituo hicho mapema mwaka huu kutawawezesha Watanzania kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Aidha amesema kuwa, Serikali imeelekeza kujengwa kwa vituo vingine vya gesi asilia, ambapo vituo saba vya ziada vinajengwa na Sekta binafsi katika Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba, Wizara ya Nishati imepanga kuanzisha vituo vinavyotembea vya kujaza gesi asilia katika Mikoa ya Morogoro na Dodoma.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema kuwa wamekubaliana na Shirika la Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuleta mabasi yanayotumia gesi asilia hatua inalenga kuhamasisha Watanzania kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuelekea kwenye Nishati safi na rafiki kwa mazingira.
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho kimetoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mradi huo, Profesa William Anangisye amefafanua kuwa, Mradi huo utatoa fursa kwa wanafunzi wanaosomea masuala ya gesi kutumia kituo hicho kama sehemu ya mafunzo ya vitendo.
KAZI INAONGEA
No comments: