LIVE STREAM ADS

Header Ads

Baraza la Madiwani Mwanza Jiji lapitisha bajeti ya mwaka 2025/26

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Mwanza limepitisha makadirio ya bajeti ya shilingi bilioni 124,378,085,328 kwa mwaka wa fedha 2025/ 2026 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Akizungumza Ijumaa February 21,2025 kwenye kikao cha Baraza hilo, Mchumi wa Halmashauri hiyo, Jeremiah Lubeleja alieleza kuwa bajeti hiyo ni ongezeko la asilimia 11.3 ikilinganishwa shilingi 110,293,332,684 kwa mwaka 2024/2025 ikiwa ni sawa na ongezeko la shilingi 14,084,752,644 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo ongezeko hilo linatokana na ruzuku ya mishahara kuongezeka.

Aidha alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi 83,006,538,000 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumisha, miradi ya maendeleo shilingi 6,065,121,084, matumizi ya kawaida shilingi 2,443,743,000, wadau wa maendeleo shilingi 3,936,058,000 na vyanzo vya ndani vya Halmashauri shilingi 28,926, 625,244.

Hata hivyo alisema Halmashauri hiyo inakadiria kukusanya Shilingi 28,278, 239,768 kwa mapato ya ndani, mapato fungiwa shilingi 5'335,642,750 na mapato yasiyofungiwa shilingi 22,942,597,018 ambapo makadirio ya makusanyo hayo yamepungua kwa kiasi cha shilingi 2,980,021,231 sawa na upungufu wa asilimia 9.5 ya makisio ya mwaka 2024/2025 ambayo yalikuwa shilingi 31,258,21,000.

Alisema mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri hiyo imepanga kutekeleza miradi ya maendeleo kama miundombinu ya barabara kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani, kuimarisha miundombinu ya elimu msingi na sekondari kwa kujenga madarasa na kutengeneza madawati, utoaji wa huduma za afya na kujenga masoko mawili mapya na kukarabati wa masoko mawili ya zamani wa lengo la kuboresha mazingira ya wafanyabiashara.

Lubeleja alisema rasimu ya mpango wa bajeti ya Halmashauri hiyo imeandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha namba 21 cha Sheria na Kanuni ya mwaka 2015 na kuzingatia dira ya Taifa ya Maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi aliwataka madiwani na watendaji wa Kata kuhakikisha wanasimamia bajeti hiyo kwa uweledi ili kutatua changamoto za wananchi na kuleta matokeo chanya.

"Kila siku nimekuwa nikisema umuhimu wa kusimamia Halmashauri, ukiwa na viongozi imara lazima utakuwa na Serikali imara na kama utakuwa na viongozi legelege basi utakuwa Serikali legelege" alisema Makilagi.

Nao baadhi ya madiwani walieleza kuwa wameridhika na bajeti hiyo kwani imegusa kila idara ambayo ina changamoto mbalimbali na itasidia kusukuma maendeleo ya Jiji la Mwanza.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi.
Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Jeremiah Lubeleja.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.