Biteko ahimiza umuhimu wa kuhifadhi misitu
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali yawaasa wananchi kutunza mazingira hususan vyanzo vya maji ili kusaidia upatikanaji wa maji nchini. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amezindua taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za maji kwa mwaka 2023/24 na kusema upatikanaji wa huduma za maji ni haki ya msingi hivyo ni muhimu kulinda vyanzo vya maji kuwezesha upatikanaji wake.
Dkt. Biteko amesema hayo jijini Dar es Salaam Machi 19, 2025 ambapo amesema pamoja na jitihada zinazoendelea jamii ina wajibu wa kuhakikisha usafi wa mazingira, kupanda miti na kuhifadi misitu ili kuendelea kupata na kutumia rasilimali maji.
"Tusipotunza vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira tutajikuta katika mtanziko mkubwa (Water Stress),” amesema na kuongeza kukosekana kwa rasilimali maji kwa baadhi ya watu kinaweza kuwa chanzo cha migogoro na machafuko katika jamii husika".
Ili kukabilikana na hali hiyo na kumwezesha kila mtanzania kupata huduma za maji na usafi wa mazingira, Dkt. Biteko alizielekeza mamlaka za maji kupunguza kiwango cha upotevu maji ili kuepusha hasara ya shilingi bilioni 114.12 iliyotokana na upotevu huo kwa mwaka huu.
Hadi sasa asilimia 84 kwa mijini na asilimia 79.6 kwa maeneo ya vijijini zimeunganishwa na huduma ya maji ambapo kuna ongezeko la asilimia 7 kutoka kipindi cha mwaka uliotangulia. KAZI INAONGEA
No comments: