Dhamira ni kuhakikisha waliojiari wananufaika na hifadhi ya jamii- NSSF
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesema katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fursa kwa Wananchi Waliojiajiri kujiunga na kuchangia NSSF ili wanufaike na huduma na mafao mbalimbali yanayotolewa.
Mshomba alisema hayo tarehe 7 Machi 2025 katika soko la Kilombero, Jijini Arusha, wakati akizungumza na Mastaa wa Mchezo wa NSSF waliojiajiri ambao ni wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, machinga, bodaboda, wasani mbalimbali, biashara nyingine ndogo ndogo (wasusi, wachuuzi wa masokoni, mamalishe na baba lishe).
"Kwa muda mrefu Mastaa wa Mchezo wa NSSF ambao ni wananchi waliojiajiri walikuwa hawanufaiki na hifadhi ya jamii kwa kujiwekea akiba, lakini Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa nafasi kwa Wananchi waliojiajiri kujiunga na kuchangia NSSF ili wanufaike na mafao yote yanayotolewa pamoja na mafao la matibabu" alisema Mshomba.
Poa Mshomba alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa kutoa nafasi kwa Wananchi Waliojiajiri kujiunga na kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi waliojiajiri kujiunga kwa wingi NSSF ili iweze kuwahifadhi wanapopata majanga kama ya uzee, maradhi na ulemavu ambapo kwa wanaojiunga na kuchangia NSSF itakuwa Staa wa Mchezo wa baadaye kwa kuwapa mafao na huduma nyingine.
Alisema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha wananchi waliojiajiri wananufaika na hifadhi ya jamii kwa kujiunga na kuchangia NSSF ambapo umewekwa utaratibu mzuri kwani huko huko waliko wakibofya *152*00# wanaweza kujiunga na kuchangia kidogo kidogo kwa siku bukubuku, kwa wiki, kwa mwezi au muhula.
Aliwashukuru Mastaa wa Mchezo wote ambao wamenufaika na elimu ya hifadhi ya jamii na kuamua kujiunga na kuchangia kwa maisha bora ya sasa na ya baadaye.
Mshomba alisema lengo la NSSF ni kuhakikisha wananchi waliojiajiri popote walipo wanapata elimu ya hifadhi ya jamii, wanajiunga na kujiwekea akiba kwani jambo hilo linaenda kuondoa umasikini nchini.
Awali Makamu Mwenyekiti wa Soko la Kilombero, Rajabu Hassan aliishukuru Serikali kupitia NSSF kwa kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa Wananchi Waliojiajiri ili waweze kujiunga na kuchangia kwa ajili ya kujenga maisha bora ya sasa na ya baadaye.
Kwa upande wake Gabriel Silayo ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji, Mipango na Miradi, alowahamasisha wananchi waliojiajiri kutumia fursa ya kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo kujiunga na kuchangia ili wanufaike na mafao yanayotolewa na NSSF.
NSSF STAA WA MCHEZO, HIFADHI SCHEME - HIFADHI YA JAMII KWA WOTE.
No comments: