Wanawake Nyamagana wawakumbuka wenye uhitaji, kuelekea Siku ya Wanawake Duniani
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi amewaongoza wanawake wa wilaya hiyo kufanya matendo ya huruma kwa kutoa mahitaji mbalimbali kwa wazee wasiojiweza, wanafunzi wa shule za msingi wenye mahitaji maalum na wanawake waliojifungua na wanaotarajia kujifungua katika hospital ya Rufaa ya Mkoa Mwanza Sekou Toure.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mahitaji hayo Jumatano Machi 05, 2025, Makilagi ameeleza kuwa jamii imekuwa ikisherehekea Siku ya Wanawake Duniani kwa kutambua na kuathimisha mchango ya wanawake na kupigania haki na usawa wa kijinsia hivyo wao wameamua kuadhimisha siku hiyo kwa kuwajali wahitaji mbalimbali.
Makilagi ameeleza kuwa siku hiyo ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 08 inatoa fursa ya kuangazia changamoto wanazokutana nazo wanawake katika nyanja mbalimbali kama vile elimu, afya, ajira na usawa wa kijinsia.
"Tumeamua kutoa mahitaji haya ili tuweze kuwashika mkono wahitaji, tutembee kwa pamoja kwa walionacho na wasiokuwa nacho ili tuwe kitu kimoja" amesema Makilagi.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza ameeleza kuwa wameamua kufanya matendo ya huruma kwa wenye mahitaji maalum kwa kutoa msaada wa vitu mbalimbali lengo likiwa ni kuwashika mkono wahitaji na kuwaonesha upendo.
Kwa upande wake Renalda Mambo ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Shirika la WoteSawa ameeleza kuwa wameamua kugawa vifaa mbalimbali ambavyo vimetolewa na wadau ikiwa ni sehemu ya matendo ya huruma katika kipindi hiki cha kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
"Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yamekuwa na lengo la kuhamasisha usawa wa kijinsia, kutambua mchango ya wanawake na kutoa fursa kwa wanawake kutambulika na kusherehekea mafanikio yao katika jamii" amesema Mambo.
Nao baadhi ya wahitaji waliopatiwa msaada huo wamewashukru wanawake wilayani Nyamagana waliojitolea na kuwakumbuka kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali kwani yatawasaidia kukabiliana na uhitaji waliokuwa nayo.
Na Chausiku Said, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi.
Baadhi ya wanawake wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa zoezi la kukabidhi mahitaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwanza Sekou Toure ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani 2025.
Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi wakikabidhi msaada wa mahitaji kwa baadhi ya wanafunzi wilayani humo.
Mahitaji mbalimbali yaliyokabidhiwa kwa watu wenye uhitaji wilayani Nyamagana ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kilele chake ni Machi 08, 2025.
No comments: