LIVE STREAM ADS

Header Ads

Halmashauri zatakiwa kuajiri watumishi wa mkataba

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Festo Dugange, imezitaka halmashauri zenye uwezo wa kiuchumi kuajiri watumishi wa mikataba ili kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa

Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini, hivi karibuni wakati akifunga mkutano wa 15 wa Taasisi ya Maboresho ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) uliofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliopo kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

“Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilitoa mwongozo maalum wa namna ya kuajiri watumishi wa mikataba na hususani wa sekta ya elimu na afya, hivyo Makatibu Tawala wa Mikoa kawasimamieni Wakurugenzi wa Halmashauri kutekeleza mwongozo huo,” Dkt. Dugange amesisitiza.

Dkt. Dugange amesema, Serikali imeleta fedha nyingi katika halmashauri ambazo zimejenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na shule na inaendelea kuajiri kwa awamu, hivyo halmashauri zinazokusanya mapato ya kutosha zinapaswa kuajiri watumishi wa mikataba ili waweze kutoa huduma kwa wananchi kupitia mbiundombinu hiyo iliyojengwa na Serikali.

Aidha, Dkt. Dugange amehimiza kuwa, siku zote Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaamini watumishi wote walio chini ya TAMISEMI wakifanya kazi kwa bidii na ufanisi, ni dhahiri kwamba kiwango cha utendaji kazi wa Serikali kitakuwa ni zaidi ya asilimia tisini kwani majukumu yanayotekelezwa na TAMISEMI yanawagusa Watanzania wengi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI Beatrice Kimoleta amesema kuwa, TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Maboresho ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) ili iweze kuwa imara na kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Kazi Inaongea
kazina Utu Tunasonga Mbele

No comments:

Powered by Blogger.