Kampuni ya Rock Solutions kuzalisha ajira zaidi ya 300
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katika kuunga mkono jitihada za Serikali za upatikanaji wa ajira nchini, kampuni ya Rock Solutions Limited imeanzisha kiwanda cha kuzalisha nyavu za usalama chini ya ardhi (Wire Mesh for Underground Support) ambacho kinatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 300 huku wananchi zaidi ya 500 wakinufaika kupitia uwekezaji huo.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa kiwanda cha Rock Solutions, Fabiani Mayenga wakati akitoa tarifa kwa Mkuu wa Mkoa Mwanza, Said Mtanda kiwandani hapo.
Alisema kiwanda hicho kimejikita katika kuzalisha vifaa vinavyotumika kwenye migodi ikiwemo nyavu za kuzuia maporomoko ya ardhi chini ya migodi.
"Kiwanda hiki kitakapokamilika kitagharimu bilioni 4.7, kwa sasa tupo kwenye hatua ya kufunga mashine na mitambo mbalimbali tunatarajia kazi hii itakamilika mwishoni mwa mwezi wa tano mwaka huu" alisema Mayenga.
Aidha aliongeza kuwa uwepo wa kiwanda hicho ni chachu ya maendeleo na ukuaji wa uchumi katika maeneo husika na taifa kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kukagua kiwanda hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alisema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kwani wanatambua mchango wao wa kusaidia kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira.
Kiwanda hicho kimejengwa katika eneo la Usagara, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments: