Barrick Bulyanhulu na Taifa Gas zaja na kampeni ya Balozi Nishati
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Ayoub Busanya, Meneja Mauzo wa Taifa Gas Kanda ya Ziwa akizungumza na Mabalozi wa Nishati safi waliopata mafunzo kupitia ushirikiano wa kampuni ya migodi ya Barrick Bulyanhulu na Taifa (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi kwa ajili ya kupikia , wa pili kulia, Kaimu Meneja Mazingira na Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo na mwanzo kulia ni Afisa wa Mgodi huo. Tukio hilo limefanyika katika Halmashauri ya Msalala , Kata ya Bugarama , Kahama Shinyanga
Kaimu Meneja Mazingira na Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Zuwena Senkondo (aliyesimama) akizungumza na mabalozi wa Nishati safi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda mazingira na baadaye makabidhiano ya mitungi ya gesi kwa mabalozi hayo katika kuadhimisha siku ya Mazingira duniani , kushoto ni Meneja Mauzo wa Taifa Gas Kanda ya Ziwa , Ayoub Busanya na kulia ni Afisa wa Barrick Bulynahulu.
Diwani wa Kata ya Bugarama, Prisca Msoma akimpa
kufuli za vizimba vya kuhifadhi mitungi ya gesi
Balozi wa Nishati ambaye baada ya mafunzo ya kuwa wakala wa gesi , Bi Pili Zuberi tayari kuanza kazi yake mpya ya uwakala wa gesi , wa kwanza kushoto ni Kaimu Meneja Mazingira na Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo na wa kwanza kulia ni Ayoub Busanya, Meneja Mauzo wa Taifa Gas Kanda ya Ziwa.
Baadhi ya mabalozi wa Nishati safi wakisikiliza mada zikitolewa kuhusu umuhimu wa nishati safi na salama kwa ajili ya kutunza mazingira na afya kabla ya kukabidhiwa mitungi hiyo.
***
Katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhimiza matumizi ya nishati safi ya gesi kwa matumizi ya kupikia Barrick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Taifa Gas zimezindua kampeni ijulikanayo kama Balozi wa Nishati katika Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga.
Kampeni hii imelenga kuwawezesha na kuwahamasisha wananchi wa Msalala kutumia gesi safi ya kupikia sambamba na kuwafanya mabalozi wa nishati hiyo katika maeneo yao.
Uzinduzi wa kampeni hiyo ambao umeenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Mazingira Dunia ambapo Wananchi walipatiwa mafunzo ya nishati safi ya kupikia na mawakala 20 ambao ni mabalozi wa nishati kupatiwa mitungi 320 ya gesi kutoka kampuni ya Taifa Gas kwa ajili ya kusaidia katika uhamasishaji.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika katika kata ya Bugarama Wilaya ya Msalala , Kahama mkoani Shinyanga , Kaimu Meneja Mazingira na Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Zuwena Senkondo amesema mgodi huo utaendelea kuhamasisha vijiji vyote vinavyouzunguka kuachana na nishati chafu kwa ajili ya matumizi ya kupikia.
Zuwena Senkondo
“Mgodi wa Barrick Bulyanhulu unajali afya za wananchi wanaouzunguka na jamii nzima kwa ujumla ndio maana programu hii ilianza na mafunzo kwa wiki kadhaa ili kuwajengea uwezo namna bora ya kutumia na sasa nyie ni mawakala wa kuuza mitungi ya gesi kwenye maeneo ya Bugarama na kakola na vijiji vya jirani na muendelee kusambaa elimu hii kwa watanzania wenzetu,” amesema Senkondo.
Ameongeza kwamba katika siku hii ya mazingira duniani ni muhimu kwa watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia.
Senkondo amesema kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye anaongoza mapinduzi haya ya kijani kwa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi na malengo mpaka 2034 asilimia 80 ya watu wawe wameondokana na matumizi ya mkaa na kuni.
Ameongeza kwamba mgodi huo utaendelea kushirikiana na Taifa Gas ili kuhakikisha kwamba watu 50,000 ambao wanazunguka mgodi huo wanaacha matumizi ya nishati chafu na kuanza kutumia nishati safi ili kulinda mazingira pamoja na afya zao.
“Tumelenga makundi karibu yote katika jamii , wakinamama , vijana na wazee ili kuhakikisha kwamba kila mtanzania anapata elimu ya matumizi ya nishati safi kwa maendeleo endelevu katika nchini,” amefafanua Senkondo.
Kwa upande wake, Ayoub Busanya , Meneja Mauzo wa Taifa Gas Kanda ya Ziwa , amesema kwamba kampuni hiyo inaunga juhudi za Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye jitihada za kuhakikisha watanzania wanaanza matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia na kulinda mazingira hapa nchini.
Ayoub Busanya
Amesema kampuni hiyo kwa kushirikiana na mgodi waliendesha mafunzo kwa wiki kadhaa kwa wananchi ambao wanazunguka mgodi huo na kupata mawakala takribani 20 ambao wamekabidhiwa mitungi hiyo ya gesi na wataanza shughuli za uawakala rasmi kwa ajili ya kupanua wigo wa matumizi ya gesi kanda ya ziwa.
“Katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani leo hii sisi tupo kwenye kilele cha matumizi ya nishati safi kwa watanzania na ni matarajio yetu kwamba mradi huu wa kuwasaidia wananchi kuacha matumizi ya mkaa na kuni utafanikiwa kwa kuunganisha nguvu zetu,” amesema Busanya.
Ameongeza kwamba thamani ya mitungi hiyo ya gesi ni zaidi Tsh 20 millioni ambapo mitungi ya kilo 6 ni 240 na mitungi ya kilo 15 ni 80 ambayo imekabidhiwa kwa mawakala hao.
Amesema lengo kuu la mradi huu ni kuhakikisha kwamba upatikanaji wa nishati safi kwa sehemu za pembezoni kwa nchini unakuwa ni rahisi ili kuweza kuwapunguza wakinamama hasa wa vjijini adha ya matumizi ya mkaa na kuni ambayo yanaathiri afya zao kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake , Diwani wa Bugarama , Prisca Msoma ameipongeza kampuni hizo kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia.
“Hizi ni juhudi kubwa kabisa za kutaka watanzania waachane na matumizi ya mkaa na kuni na kuingia kwenye mapinduzi ya kijani kwa kutumia nishati safi na salama ambayo ni bora kwa mazingira ,” amesema Msoma.
Naye , Pili Zuberi mmoja wa mawakala aliyepata mafunzo hayo amesema ni hatua muhimu kwa jamii ya watanzania kuanza matumizi ya nishati safi kwa ajili ya matumizi ya kupikia na kulinda mazingira na afya.

No comments: