LIVE STREAM ADS

Header Ads

TGNP Yafanya Mdahalo Ngazi ya Mkoa wa Usawa wa Kijinsia na Mapambano Dhidi ya Ukatili

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Na Mwandishi Wetu – Dodoma

Katika jitihada za kuendeleza usawa wa kijinsia na kumaliza vitendo vya ukatili, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia mradi wake wa Tuinuke Pamoja, umefanikiwa kuandaa mdahalo wa ngazi ya mkoa uliowakutanisha wadau kutoka halmashauri tatu za Mkoa wa Dodoma: Chemba, Kondoa Mji na Kondoa DC. Mdahalo huo ulifanyika katika kata tatu ambazo zinatekeleza mradi huo: Kidoka (Chemba), Suruke (Kondoa Mji) na Keikei (Kondoa DC).

Mdahalo huo wa jamii uliwaleta pamoja wazee wa mila, viongozi wa dini, wawakilishi wa vikundi vya kijamii, wanavituo vya taarifa na maarifa pamoja na viongozi wa vijiji na kata. Lengo kuu lilikuwa kuibua changamoto na kuweka mikakati ya pamoja katika kufanikisha usawa wa kijinsia, kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, na kupambana na ukatili wa kijinsia.

Miongoni mwa changamoto kubwa zilizoibuliwa ni mfumo wa umiliki wa ardhi unaowabagua wanawake. "Ardhi inamilikiwa zaidi na wanaume. Wanawake hawapati haki sawa hata kama wanashiriki kwenye uzalishaji," alisema mmoja wa washiriki kutoka Keikei.

Masuala mengine ni wanawake kubaki nyumbani na kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, watoto wa kike kunyimwa fursa ya elimu, na ndoa za utotoni zinazochochewa na mila potofu na umasikini. Kwa mfano, jamii za Wagogo na Waburungi hutoa ng’ombe 8 kama mahari na hali hii imekuwa kichocheo kikubwa cha mimba na ndoa za utotoni.

Shule pia zimegubikwa na changamoto kama utoro kutokana na uhaba wa chakula, mimba za utotoni, uwiano duni wa matundu ya vyoo, ukosefu wa taulo za kike, na udumavu wa watoto. Katika shule ya msingi Kidoka, kuna wanafunzi 1,500 lakini matundu ya vyoo ni 7 kwa wavulana na 14 kwa wasichana, hali inayokwenda kinyume na sera inayotaka uwiano wa 1:20 kwa wasichana na 1:25 kwa wavulana.

Rushwa ya ngono kwenye nafasi za uongozi na vikao mbalimbali, ubakaji kwenye maeneo ya starehe, na ukatili wa kimwili na kijinsia pia vilitajwa kuwa changamoto kubwa. Kesi nyingi haziripotiwi kwa polisi kutokana na ukosefu wa vituo vya karibu, uelewa mdogo wa sheria, na mila za kulindana.

"Familia nyingi hutatua kesi za ukatili majumbani kwa kutoa fidia ya ng’ombe au pesa, jambo linalonyima haki wahanga wa ukatili," alisema mmoja wa viongozi wa kituo cha maarifa.

Pia ilibainika kuwa jamii nyingi zinaendelea kushikilia mila na desturi kandamizi kama urithi wa wajane, mgawanyo usio sawa wa mirathi, na dhana potofu kuwa umasikini ni mpango wa Mungu.

Washiriki wa mdahalo walipendekeza kuimarisha utoaji wa elimu kwa makundi rika na jamii kwa ujumla. Midahalo ya wanaume na wanawake inapaswa kuendelea katika vijiji na vitongoji ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Viongozi na mgambo wasimamie utekelezaji wa masharti ya kuendesha ngoma za usiku ili kuzuia ushiriki wa watoto na matukio ya ukatili. Serikali ijenge vituo vya polisi katika kata husika ili kurahisisha ufuatiliaji wa sheria na kuhakikisha haki inatendeka.

Elimu ya haki za binadamu na utaratibu wa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia inapaswa kutolewa kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa kulinda haki zao. Wazazi na jamii kwa ujumla waelimishwe kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike na madhara ya ndoa za utotoni.

Miongozo ya serikali kuhusu mila kama jando na unyago ishushwe hadi ngazi ya jamii. Kesi za jinai zihamishiwe kwenye vyombo halali vya utoaji haki badala ya kumalizwa nyumbani au kwa viongozi wa dini.

Halmashauri za vijiji zihakikishe kila kitongoji kinapata maji safi na salama, huku juhudi zikiwekwa katika kuzuia mimba na ubakaji wa watoto wa kike. Viongozi wa dini wahusike moja kwa moja katika uthibitishaji wa umri wa wanaoolewa ili kuzuia ndoa za utotoni, na kuhakikisha ndoa zote zinafuata taratibu za kisheria.

Elimu ya jinsia kwa viongozi wa dini ipewe kipaumbele, ili wawe mabalozi wa mabadiliko chanya ndani ya jamii na kupunguza upinzani dhidi ya ajenda ya usawa wa kijinsia. Maamuzi ya matumizi ya mali ya familia, hususan mazao, yashirikishe wanawake ili kuepusha matumizi holela na unyonyaji.

Upatikanaji wa huduma za afya, hasa vituo vya afya na zahanati, uboreshwe katika vijiji husika ili wanawake wajifungue salama. Elimu ya jinsia itolewe kwa mashehe, maimamu na viongozi wengine wa dini kwa kushirikiana na TGNP, ili kusaidia jamii kuibua miradi ya maendeleo yenye mtazamo wa kijinsia inayoweza kuingizwa katika mipango ya bajeti ya serikali za mitaa.

Mhe. Elizabeth Kaiza, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Kondoa Mjini alisema:

“Suala la ukatili wa kijinsia linahitaji elimu na ushirikiano mkubwa. Mahakama haiwezi kufanya kazi peke yake bila ushahidi na ushirikiano wa wazazi na jamii. Kesi nyingi hupotea kwa sababu watu wanamaliza nyumbani au hawaleti mashahidi.”

Kwa upande wake, Mkaguzi Asha Omary kutoka Dawati la Jinsia na Mtoto, Polisi Kondoa alisema: “Rushwa ya ngono ni ukatili wa kijinsia. Tujitambue na tusikubali kudhalilishwa kwa njia yoyote. Haki haipaswi kununuliwa kwa hongo ya mwili.”

Elizabeth Shoo, Afisa Maendeleo na Mratibu wa Mradi wa Tuinuke Pamoja Kondoa DC alisema:“Mradi huu una nafasi ya kuleta mabadiliko chanya endapo kutakuwa na mshikamano kati ya wataalam, viongozi wa vijiji na wanachama wa vikundi vya kijamii. Tuwatumie wataalam wetu walioko ngazi ya vijiji na kata, hasa kwenye elimu ya afya ya uzazi na mimba za utotoni.”

Rose Kitundu, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba alisisitiza kuwa:

“Ushirikiano wa serikali za mitaa na jamii ni muhimu sana katika kupambana na ukatili wa kijinsia. Hatufanikiwi kama kila mmoja hatabeba jukumu lake.”

Mdahalo huu ni ushahidi kuwa mradi wa Tuinuke Pamoja unaendelea kujikita kwenye mizizi ya jamii kwa kuhamasisha mijadala jumuishi, kuibua changamoto halisi, na kuweka mikakati madhubuti ya kuzitatua kwa njia shirikishi na endelevu. TGNP inaendelea kuthibitisha kuwa mabadiliko yanawezekana endapo jamii itashirikishwa kikamilifu.

No comments:

Powered by Blogger.