RC Chacha aitaka TMDA Kudhibiti Biashara Haramu ya Dawa na Vifaa Tiba
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com


Na Julius Anaclet, Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Paul Chacha, ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wananchi na wafanyabiashara wanaokiuka sheria kwa kuuza dawa na vifaa tiba bandia au visivyo salama.

Ametoa wito huo wakati wa kikao kazi kilichofanyika mkoani Tabora, kikihusisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari pamoja na viongozi wa sekta ya afya.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Chacha alisisitiza kuwa afya ya Watanzania ni kipaumbele kikuu kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alisema kuwa mapambano dhidi ya bidhaa feki ni ya lazima ili kuhakikisha usalama wa wananchi na kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma za afya nchini.
"TMDA iendelee kusimamia kwa nguvu sheria na kanuni zilizopo ili kuwabana wanaouza dawa na vifaa tiba bandia. Tunahitaji jamii yenye afya njema, na hilo linawezekana kwa kudhibiti bidhaa hafifu na zisizokidhi viwango,” alisema RC Chacha.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Honoratha Rutatinisibwa, ambaye alimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa huo, alieleza kuwa mkoa umejipanga vyema kukagua na kudhibiti usambazaji wa vifaa tiba visivyokidhi viwango. Alieleza kuwa juhudi zinaendelea ili kuhakikisha afya ya jamii inalindwa ipasavyo kupitia ukaguzi wa mara kwa mara na ufuatiliaji wa karibu wa wauzaji wa bidhaa hizo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw. Adam Fimbo (pichani), alieleza kuwa kikao kazi hicho ni sehemu ya mikakati ya mamlaka hiyo katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba. Aliongeza kuwa TMDA inaendelea kuboresha mifumo ya kidijitali kwa ajili ya utoaji wa vibali na ufuatiliaji wa bidhaa zinazohusika na afya ya jamii.
"Elimu kwa jamii ndiyo msingi wa udhibiti wa matumizi mabaya ya dawa na vifaa tiba. Pia, matumizi ya teknolojia yamekuwa chachu ya kuboresha utoaji wa vibali kwa ufanisi na uwazi," alisema Bw. Fimbo.

Katika hatua nyingine, TMDA iliwatambua na kuwatuza waandishi wa habari waliotoa mchango mkubwa kwa kuandika na kuripoti habari zinazohusu dawa na vifaa tiba. Miongoni mwa waliotunukiwa ni Bi Joyce Shebe kutoka Clouds Media, ambaye alipokea tuzo maalum kwa uandishi wenye mchango wa kielimu na kijamii.
Kikao kazi hicho kilifanyika katika muktadha wa kuimarisha ushirikiano kati ya TMDA na vyombo vya habari, kwa lengo la kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii kuhusu usalama wa dawa, vifaa tiba na umuhimu wa kufuata taratibu zilizowekwa.
No comments: