Serikali Yaanzisha Mpango Maalum Kuwawezesha Wanawake na Vijana Katika Uchimbaji Endelevu wa Madini
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com


Lengo ni Kuchochea Maendeleo, Usalama na Utunzaji wa Mazingira kwa Vizazi Vijavyo
📍Singida, Julai 17, 2025
Serikali kupitia Tume ya Madini imezindua mpango maalum wa “Uchimbaji Bora na Endelevu kwa Kizazi Kijacho”, unaolenga kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchimbaji madini nchini. Mpango huu unatoa fursa ya kuanzisha vikundi, kupata mikopo, pamoja na leseni za uchimbaji kwa lengo la kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika mafunzo kwa wachimbaji wadogo yaliyofanyika katika vijiji vya Utaho A na Isalanda, Kata ya Kituntu na Puma mkoani Singida, Mjiolojia kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Mutagwa, amebainisha kuwa mpango huo pia unalenga kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa usalama na kuzingatia utunzaji wa mazingira.
“Uchimbaji salama ni msingi wa maendeleo. Tunawafundisha wachimbaji si tu kuhusu mbinu bora za uchimbaji, bali pia umuhimu wa kulipa kodi ya serikali kama vile mrabaha wa asilimia 4 kwa madini ya ujenzi,” amesema Mutagwa.
Aidha, amewaonya wanaojihusisha na ununuzi wa madini bila kulipa kodi, akisisitiza kuwa mfumo wa malipo ya kodi unapatikana kupitia POS katika ofisi za madini.
Amesisitiza kuwa kila mchimbaji ana wajibu wa kutoa taarifa za ukwepaji kodi kwa mujibu wa Kifungu cha 87 cha Sheria ya Madini, Sura ya 23, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Migodi na Baruti kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Eng. Lameck Maduhu, amesisitiza umuhimu wa usalama katika maeneo ya kazi.
“Fedha tunazopata zitakuwa hazina maana kama hatutajilinda. Ni lazima kuvaa vifaa kinga muda wote – safety boots, kofia ngumu, suruali maalum na barakoa. Ndala hazihusiki kabisa kwenye machimbo,” ameeleza kwa msisitizo.
Ameongeza kuwa uchimbaji unaozingatia matumizi ya baruti unapaswa kufanywa kwa njia ya kitaalam na kwa uangalifu mkubwa ili kuzuia uharibifu wa mazingira, akihimiza wachimbaji kuacha tabia ya kukata na kuchoma miti kiholela.
Mchimbaji wa madini ya ujenzi kutoka Kijiji cha Utaho A, Jenifa Mtandu, ameishukuru Tume ya Madini kwa elimu waliyopewa, akisema imewapa maarifa ya kujilinda, umuhimu wa vikundi, na fursa za kupata mikopo kwa maendeleo ya shughuli zao.
“Mafunzo haya yametufungua macho. Tunajua sasa umuhimu wa leseni, kuwa na vikundi na mikopo. Tunaiona kesho yetu ikiwa salama zaidi,” amesema Mtandu kwa furaha.
Mpango huu umewezeshwa kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa lengo la kusaidia wachimbaji wadogo wa madini ya ujenzi hususan kokoto, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya miundombinu, kuongeza kipato na kuchangia mapambano dhidi ya umasikini katika jamii.

No comments: