LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanawake Wasema ‘Tupo Tayari’, Sasa Ni Zamu ya Vyama Kuwapa Majimbo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Wadau wa masuala ya wanawake na uongozi wamevitaka vyama vya siasa nchini kuhakikisha vinawateua wanawake waliokidhi vigezo kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, hususan kwenye nafasi za uwakilishi, ubunge na udiwani zinazoshindaniwa majimboni.

Wakizungumza katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, wadau hao wameeleza kuwa kwa muda mrefu wanawake wamekuwa wakipewa nafasi za viti maalum pekee, hatua inayowanyima nafasi ya kushindana moja kwa moja na wanaume na kuonesha uwezo wao katika siasa za ushindani.

Katika kipindi hiki cha mchakato wa chaguzi za ndani ya vyama kuelekea uchaguzi mkuu, wanawake wengi wamejitokeza kuchukua fomu, licha ya kuwa idadi yao bado ni ndogo kulinganisha na wanaume.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu Zanzibar, wanachama 1,640 wamechukua na kurejesha fomu za kugombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani, ambapo kati yao wanawake ni 406, sawa na asilimia 24.7.

Chama cha ACT Wazalendo kwa upande wake kimeripoti kuwa kati ya wanachama 435 waliotangaza nia ya kugombea nafasi hizo visiwani humo, wanawake ni 40 pekee, sawa na asilimia 9.2.

Vyama hivyo vinasubiri vikao vya Kamati Kuu na Kamati Maalum kupitisha rasmi majina ya wagombea, mchakato unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Julai hadi Agosti 2025.

Wadau wametoa pongezi kwa wanawake hao kwa ujasiri wa kujitokeza lakini wakasisitiza kuwa hatua hiyo haitoshi iwapo hawatapewa nafasi halisi ya kugombea majimboni.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Zanzibar ilifanikiwa kupata wanawake wanane pekee (sawa na asilimia 16) katika Baraza la Wawakilishi na wabunge wanne (asilimia 8), kupitia siasa za ushindani.

“Tunaomba wajumbe wa vikao vya uteuzi kwenye vyama mbalimbali kuwapigia kura wanawake wakati wa mchakato wa kuwapata wagombea wa mwisho. Huu ni wakati wa kufanya mabadiliko halisi ya kisiasa na kijamii kwa kuzingatia usawa wa kijinsia,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Wadau wamesisitiza kuwa uwepo wa wanawake kwenye nafasi za juu za uongozi ni chachu ya maendeleo ya taifa, kwani tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa wanawake ni viongozi waadilifu, wanaoweka mbele maslahi ya familia na jamii, na ni wasikivu na wenye kujitoa.

Wakirejea Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) wa mwaka 1979, wadau hao wamekumbusha wajibu wa Tanzania kama nchi mwanachama kuhakikisha inachukua hatua za kuongeza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi.

Taarifa hiyo imetolewa kwa ushirikiano wa taasisi kadhaa za wanawake zikiwemo Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway.

Wamewatia moyo wanawake waliotia nia wasikate tamaa bali waendelee kuwa imara na waaminifu kwa dhamira ya uongozi kwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.











No comments:

Powered by Blogger.