SERIKALI KUVUNA ASILIMIA 20 MGODI MPYA WA NYANZAGA MWANZA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Tarehe 20 Agosti 2025 Serikali na kampuni ya Nyanzaga Mining company limited kwa pamoja walisaini makubaliano ya nyongeza kwa ajili ya uchimbaji mkubwa wa madini aina ya dhahabu kupitia kampuni ya ubia ya Sotta Mining corporation limited.
Akizungumza na wananchi kwenye hafla ya utiaji saini katika kijiji cha Sota-Igalula Wilayani Sengerema, Waziri wa Madini Mhe. Anthoy Mavunde alisema nyongeza hiyo ya makubaliano ya hisa zisizofifishwa utaongeza hisa 4% kwa serikali kutoka 16% hadi 20% huku hisa za mwekezaji zikishuka kutoka 84 hadi 80% kutoka katika mkataba wa awali.
Mhe. Mavunde alisema uwekezaji kwa ujumla ni wa zaidi ya Tshs. Trilioni 1 na kwa kupitia nyongeza hiyo serikali itanufaika na nyongeza ya kodi kutokana na faida ya kiuchumi ya uchimbaji na kwa kupitia miradi miambata pia serikali itanufaika na kodi, tozo, mirabaha, na ushuru mwingine wowote utakaowekwa na wakala wa serikali.
“Mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa kwa sasa ni asilimia 10.1 kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya muda uliopangwa, Makusanyo yote ya Maduhuli kwa 2015/16 yalikua ni Bilioni 162 lakini tarehe 30 Juni 2025 tumeingiza Trilioni 1.7 sawa na asilimia 103 ya lengo na tuna akiba kubwa ya dhahabu ya tani 8.7 iliyokusanywa ndani ya miezi 9 pekee na tayari tuna viwanda 8 vya kusafisha madini ya dhahabu kwa viwango vya 99.9” alisema Mhe. Mavunde.
Naye Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. Said Mtanda alisema kupitia mgodi huo maisha ya wananchi wa sengerema na Mwanza kwa ujumla yatainuka kiuchumi na kusaidia uchangiaji wa pato la taifa kwa wastani wa kutoka 7.5% ya sasa hadi 10% ikiwa ndio malengo ambayo mkoa umejipangia.
Mkurugenzi wa kampuni tanzu ya Perseus Mining na Nyanzaga Co Ltd. Bi. Liame De brune aliahidi kuwa kampuni ya Nyanzaga itafuata sheria na taratibu zote za nchi katika kuhakikisha mradi unasonga mbele kwa maslahi ya pande zote mbili na kwamba wana imani kuwa dhahabu ya kwanza itapatikana katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2027.
No comments: