LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kibaha Mjini: Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi waanza Mafunzo Rasmi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com






Na Mwandishi Wetu, Kibaha

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imeanza rasmi mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata, ikiwa ni sehemu ya maandalizi muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Mafunzo hayo yamezinduliwa rasmi tarehe 4 Agosti 2025 na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kibaha Mjini, Bi. Theresia Kyara, ambaye aliwahimiza washiriki kuwa makini, kushiriki kikamilifu na kuhakikisha wanazingatia katiba, sheria, kanuni na miongozo yote ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

“Ni muhimu msikie kwa makini, mzingatie Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria na miongozo ya Tume. Majukumu yenu ni nyeti na yanahitaji weledi, uadilifu na uaminifu mkubwa,” alieleza Bi. Kyara mbele ya washiriki wa mafunzo hayo.

Kabla ya kuanza kwa mafunzo, washiriki wote waliapishwa rasmi na Mheshimiwa Frederick U. Shayo kutoka Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, hatua muhimu ya kisheria inayowatambulisha rasmi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi.

Mafunzo haya ya siku tatu yanatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 4 hadi 6 Agosti 2025 yakijumuisha mada mbalimbali zinazolenga kuwajengea uwezo wahusika katika kusimamia ipasavyo zoezi la uchaguzi katika ngazi ya kata.

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani umepangwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025, chini ya kaulimbiu:
“Kura Yako, Hakika Yako – Jitokeze Kupiga!”

No comments:

Powered by Blogger.